Simba SC, Namungo zaweka historia nchini

27Feb 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba SC, Namungo zaweka historia nchini

HISTORIA imeandikwa nchini kwa timu mbili za Tanzania kutinga hatua za makundi ya makombe makubwa barani Afrika kwa wakati mmoja, baada ya juzi Namungo FC kufanikiwa kufuzu hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika, CAF.

Namungo, pamoja na kuchapwa mabao 3-1 na timu ya Clube Desportivo Primeiro de Agosto ya Angola, imefuzu kwa jumla ya mabao 7-5 kutokana na kushinda mabao 6-2 kwenye mchezo wa awali.

Michezo yote ilichezwa nchini Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, wa kwanza ukihesabika kuwa ni wa ugenini, baada ya timu hiyo kuzuiliwa kuingia nchini Angola kwa kile walichodai ni kuzuia kuenea maambukizo ya virusi vya corona.

Namungo inaungana na Simba ambao tayari ilikuwa imeshatinga hatua ya makundi na tayari imeshacheza mechi mbili dhidi ya AS Vita ya Congo DR na Al Ahly ya Misri na zote kushinda kwa bao 1-0.

Hii ni mara ya kwanza kwenye historia ya soka la Tanzania kwa timu zake zote mbili kuweza kuingia hatua ya makundi ya makombe hayo makubwa Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa wakati mmoja.

Wakati Simba inaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa kwenye Kundi A na timu za AS Vita, Al Ahly na El Merreikh ya Sudan, Namungo yenyewe ipo Kundi D, ikiwa na timu za Nkana FC ya Zambia, Pyramids ya Misri, na Raja Casablanca ya Morocco.

Habari Kubwa