Simba SC, Yanga zachanga karata

25Mar 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba SC, Yanga zachanga karata

LICHA ya kuwa tayari kukata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa, Simba na Yanga zinaendelea kujiimarisha ili kuhakikisha zinamaliza kwa heshima mechi za makundi za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

 

Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Machi 31, mwaka huu itakuwa Morocco kuwafuata Raja Casablanca wakati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itawaalika Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema viongozi wa klabu hiyo wamekutana na benchi la ufundi kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kufanya vyema mchezo wa robo fainali.

Hersi alisema wanataka kuona wanashinda mechi hiyo ya kukamilisha hatua ya makundi kwa sababu itawaongezea nguvu katika hatua inayofuata.

“Tunahitaji kufanya vizuri mechi hiyo na  kumaliza kundi tukiendelea kuongoza ili katika hatua inayofuata tupate angalau mpinzani mwenye uwezo wa kawaida. Tayari tumejiandaa kuelekea mchezo huo lakini pia na kuweka mipango yetu ya mechi ijayo ya hatua ya robo fainali, nina imani kuna mambo mazuri na makubwa yanakuja ndani ya klabu yetu,” alisema Hersi.

Mshambuliaji wa Yanga,  Fiston Mayele, amesema anafurahi kuona amekuwa na msaada mkubwa katika timu yake kuelekea hatua ya robo fainali huku bao lake alilofunga dhidi ya US Monastir ya Tunisia likitangazwa ni goli bora la mzunguko wa tano.

“Kwa sasa niko katika majukumu ya Timu ya Taifa, baada ya michezo hiyo nitaungana na kikosi cha Yanga ambao nitawakuta nyumbani (DRC) kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe, ni muhimu kupata matokeo mbele ya wenyeji wetu,” alisema Mayele.

Aliongeza wanafahamu mechi hiyo itakayochezwa Aprili 2, mwaka huu Mjini Lubumbashi itakuwa ngumu kwa sababu wao wataingia na rekodi ya kushinda mechi ya kwanza.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kimeanza mazoezi rasmi kujiwinda kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Raja Casablanca.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba,  Ahmed Ally, alisema wachezaji wote ambao hawako katika timu za taifa wameanza kujifua kujiandaa na mchezo huo wa kukamilisha ratiba lakini muhimu kuelekea hatua inayofuata.

“Tunatambua mchezo utakuwa mgumu sana kwa ubora wa wapinzani wetu, hatutaenda kinyonge katika mechi hiyo, kwa sababu tunahitaji kutafuta angalau alama moja,” alisema Ahmed.

Aliongeza kama ilivyo kawaida yao, wametanguliza ofisa ambaye anakwenda kuandaa mazingira bora ya mahali timu itakapofikia na maandalizi mengine muhimu ambayo wanalenga kupata matokeo chanya.