Simba SC yasisitiza kumkataa Kilomoni

17Jul 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Simba SC yasisitiza kumkataa Kilomoni
  • *** Magori aonyesha barua kutoka Rita, mwenyewe aziruka nyaraka hizo...

KUFUATIA kuzungumza taarifa mbalimbali zinazotofautiana uamuzi uliofanyika wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji, uongozi wa Simba umesema kuwa, Hamisi Kilomoni si mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, imeelezwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori.

Hata hivyo Kilomoni ameibuka na kusisitiza kuwa bado anatambua yeye ni mdhamini wa klabu hiyo, kwa sababu hajapata barua yoyote inayobatilisha uteuzi wake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema kuwa Kilomoni aliondolewa rasmi kwenye orodha ya wadhamini wa klabu hiyo tangu Oktoba 12 mwaka 2017 na anakosea kuendelea kujitambulisha kwamba yeye ni mdhamini.

Magori alisema kuwa mzee Kilomoni alivuliwa ujumbe wa bodi ya wadhamini na kitendo cha kuendelea kujitangaza kwamba bado ni mdhamini ni kosa.

Alisema kuwa klabu ilitoa taarifa za mabadiliko hayo kwa wakili beki huyo wa zamani wa Simba na wanachomtaka ni kutulia ili asichukuliwe hatua zaidi za kinidhamu.

"Barua zote tunazo hapa na nimekuja nazo, napenda kuwaambia wanachama kuwa suala la mzee huyu (Kilomoni), tunalifunga rasmi leo (jana)," alisema Magori.

Alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo umeamua kulipeleka suala la Kilomoni kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili achukuliwe hatua.

Kilomoni aliliambia gazeti hili kuwa hajawahi kupata barua yoyote kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Michezo inayoeleza kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

"Si mimi wala wakili wangu aliyeandikiwa barua hiyo, hizo taarifa si za kweli, na wanazidi kukoroga mambo hao watu (viongozi wa Simba), mimi nitatoa taarifa wiki ijayo kujibu hayo waliyoyasema," alisema Kilomoni.

Wakati huo huo, Simba ilitangaza rasmi kuongeza jezi ya tatu ambayo itaanza kutumika katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni rangi ya kijivu.

Magori alisema uamuzi huo unazingatia kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika mashindano yake, kila timu kuwa na jezi huru isiyofungamana.

"Kwa miaka mingi imezoeleka jezi zetu za nyumbani ni nyekundu na nyeupe kwa michezo ya ugenini, jezi za kijivu tutazitumia pale ambapo jezi zetu zitagongana kwenye mchezo na timu pinzani," alisema Magori.

Aliongeza kuwa Simba imekamilisha usajili wake kwa asilimia 90 na kutaja idadi ya wachezaji waliosaini mikataba ni 26, huku akisema kwamba nafasi moja iliyobakia ili kukamilisha kikosi cha watu 27 wataijaza hivi karibuni kama walivyokusudia.