Simba, Stand mechi ya kisasi leo

13Feb 2016
WAANDISHI WETU
SHINYANGA
Nipashe
Simba, Stand mechi ya kisasi leo

SIMBA itaingia vitani na Azam FC kuwania kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakaposhuka kwenye Uwanja wa Kambarage mjini hapa leo jioni kuikabili Stand United inayosaka kisasi cha kufungwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam duru la kwanza msimu huu.

WACHEZAJI WA TIMU YA STAND UNITED

Simba itahitaji ushindi kukaa kileleni mwa msimamo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13, ambao Yanga walitwaa ubingwa licha ya kuanza vibaya kwa suluhu dhidi ya Prisons na vichapo vya 3-0 na 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Kikosi cha Jackson Mayanja pia kitakwea kileleni kikitoka sare leo ikiwa Azam FC watapoteza au kushikwa kwa sare ugenini dhidi ya Coastal Union jijini Tanga.

Timu zilizokuwa zikibadilishana kukaa kileleni msimu uliopita ni Mtibwa, Azam na Yanga ambao mwishoni mwa msimu waliziacha kwa mbali timu nyingine na kutwaa ubingwa wakiwa na mechi mbili mkononi.

Kabla ya kuanza kwa mazoezi ya kikosi chake jana, Mayanja aliiambia Nipashe mjini hapa kuwa anaamini hataangushwa na safu yake ya ushambuliaji inayoundwa na Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu, Hajji Ugando na Danny Lyanga.

Safu hiyo imefutupia kwenye nyavu mara 16 katika mechi zote sita, ambazo Simba imecheza chini ya kocha mkuu huyo mpya tangu kutimuliwa Dylan Kerr Januari 10.

"Hapa (Shinyanga) ni ngumu kupata ushindi, lakini tumejipanga, tuna wachezaji wazuri kuanzia nyuma hadi mbele, naamini hawatatuangusha," alisema Mayanja ambaye tangu apewe mikoba ya Kerr, Simba imeruhusu bao moja tu katika mechi zote sita ilizocheza chini yake.

Mbali na kupigania kukaa kileleni mwa msimamo wa VPL, Simba pia itasaka ushindi ili kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 dhidi ya Stand iliyokuwa imebaki na wachezaji tisa baada ya nyota wake kulimwa kadi nyekundu katika mechi yao ya duru la pili msimu uliopita mjini hapa.

Stand inayokamata nafasi ya tano kwenye msimamo, ina mechi moja ya kiporo dhidi ya Azam FC, itaingia uwanjani leo ikiwa na rekodi ya kutopata sare nyumbani katika mechi zote tisa ilizocheza mjini hapa msimu huu.

Kikosi cha Mfaransa Patrick Liewig kimeshinda sita na kupoteza tatu dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam FC na Mwadui FC. Katika mechi hizo tisa, 'wapigadebe wa stendi' wametupia mara 12 na kufungwa magoli matano.

Wapinzani wao wa leo (Simba) hadi sasa wamecheza mechi nane nje ya jiji la Dar es Salaam wakishinda tano, sare mbili na kupoteza moja, huku wakifunga mabao nane na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.

"Kila mechi ya ni muhimu kwa sababu hii ni ligi. Nililazimika kuipeleka timu mahali tulivu ili kila mchezaji aelekeze mawazo kwenye mechi yetu ya kesho (leo) kama tulivyofanya katika mechi zilizopita," Liewig aliwaambia waandishi wetu jana mchana.

Habari Kubwa