Simba straika tishio, Waarabu beki kisiki

11Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Simba straika tishio, Waarabu beki kisiki
  • ***Takwimu zinatisha kila upande kwa safu ya ulinzi ikionyesha ni mechi ngumu kwa...

WAKATI kikosi cha Simba kikijiandaa kuivaa JS Saoura Jumamosi, safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara ni tishio zaidi ukilinganisha na ya Waarabu hao wa Algeria ambao pia ni wazuri katika ulinzi, imefahamika.

Simba ambayo imerejea jijini Dar es Salaam juzi ikitokea Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi, itaialika JS Saoura katika Uwanja wa Taifa Jumamosi saa 10 jioni hiyo ikiwa ni mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi.

Tayari Kocha wa Simba, Patrick Aussems alishasema hataki kufanya makosa katika mechi zake za nyumbani na kwamba anaamini kikosi chake kimeiva vya kutosha kuweza kupambana.

Aussems aliliambia Nipashe kuwa anataka kuona timu yake ikifika mbali katika michuano hiyo na hilo wamejipanga kulitekeleza.

"Malengo yetu ni kwenye Ligi ya Mabingwa, tunataka kuhakikisha tunafanya vizuri na kufika mbali," alisema Aussems.

Hata hivyo, wakati wawakilishi hao pekee wa Afrika Mashabiki na Kati, Simba wakijiandaa kwa mechi hiyo dhidi ya Waalgeria, takwimu zinaonyesha JS Saoura ni imara katika safu ya ulinzi, na Wekundu wa Msimbazi wakifunika kwa ushambuliaji, ingawa pia beki yao ikionekana pia kuwa imara.

Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria 'Ligue 1', inayoshirikisha timu 16, hadi sasa mechi 16 zikiwa zimeshachezwa kwa kila timu, kwenye timu tano zilizoko tano bora, JS Saoura ni timu pekee iliyoruhusu mabao machache zaidi lakini pia ikifunga machache.

JS Saoura ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 23 katika msimamo huo unaoongozwa na USM Alger yenye alama 33 ikifuatiwa na JS Kabylie pointi 29 na ES Setif yenye alama 24 sawa na MC Alger.

Hadi sasa JS Saoura imeziona nyavu mara 14 tu katika mechi 16 ambayo ni sawa na wastani bao 0.87 kwa mechi.

Kwa upande wa Simba iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara inayoshirikisha timu 20, yenyewe ina pointi 33 katika mechi 14 huku ikiwa na michezo minne mkononi dhidi ya vinara Yanga wenye alama 50 kutokana na michezo 18.

Hata hivyo, hadi sasa Simba imetupia mabao 28 ambayo ni sawa na wastani wa mabao mawili kwa kila mechi, jambo linaloonyesha safu yake ya ushambuliaji ni hatari kuliko ya JS Saoura.

Kwa upade wa safu ya ulinzi, pia Simba ipo imara kwani ndiyo iliyofungwa mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa JS Saoura katika Ligi Kuu Algeria.

Hadi sasa Simba imeruhusu mabao matano tu katika mechi 14, wakati JS Saoura yenyewe ikiruhusu mabao saba kutoka katika mechi 16.

Aidha, hadi sasa katika mechi za Ligi Kuu, Simba imeshinda mechi 10, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja, wakati JS Saoura imeshinda sita, sare tano na kupoteza mechi tano.

Na katika mechi tatu za Ligi Kuu zilizopita, JS Saoura imepoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya JS Kabylie kisha ikatoka sare tasa nyumbani dhidi ya Olympique ikiwa ni baada ya kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya ES Setif.

Kwa upande wa Simba ambayo imetoka kushinda mechi tatu mfululizo za Kombe la Mapinduzi, kwenye Ligi Kuu michezo mitatu iliyopita imeshinda 2-1 dhidi ya KMC baada ya kuichapa 3-0 Singida United ikitoka kumaliza sare tasa dhidi ya Lipuli, mechi zote ikicheza nyumbani Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa