Simba: Tulistahili ushindi

25Feb 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Tulistahili ushindi

WAMEKAA! Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema kikosi chake kilistahili kupata ushindi katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kutoka Misri kwa sababu wachezaji wake walicheza mpira kwa nidhamu ya hali ya juu.

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 na kufikisha pointi sita ambazo zimewafanya wawe vinara katika Kundi A wakifuatiwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Al Ahly na Al Merrikh ya Sudan ambayo haina pointi inaburuza mkia.

Gomes aliliambia gazeti hili nidhamu hiyo ya mechi iliwasaidia kupata matokeo chanya katika mchezo huo wa pili katika hatua ya makundi ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mfaransa huyo alisema ameridhishwa na uwezo walioonyesha wachezaji wake katika mchezo huo na namna walivyopambana kulinda bao ambalo walilipata kupitia Luis Miquissone.

"Nimefurahi kupata ushindi wa bao 1-0, matokeo haya tumeweza kuongeza pointi na sasa kuwa na alama sita, hii ni ishara nzuri kwetu, kuelekea mechi zetu zijazo tunaamini pia zitakuwa ngumu na zenye ushindani mkubwa," alisema Gomes.

Kocha huyo pia aliwapongeza wachezaji wake kufanya kile alichowaelekeza licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali katika mchezo huo, lakini muhimu walifanikiwa kila mmoja kutimiza majukumu yake ambayo aliwapa wakiwa kwenye mazoezi.

Naye Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane, aliipongeza Simba kwa ushindi waliopata na kusema anaamini hawajafungwa kwa kuzidiwa mbinu bali hali ya hewa ya joto haikuwa rafiki kwa wachezaji wake.

Mosimane alisema walijitahidi namna ya kucheza na wapinzani wao, lakini ilishindikana kwa sababu ya changamoto hiyo ya hali ya hewa.

"Tulicheza mpira mzuri, tulijitahidi kwenda na wapinzani wetu na hili tulijua tangu awali jambo ambalo lilitufanya nasi tuongeze juhudi ndani ya uwanja, hatujapoteza kimbinu ila hali ya hewa muda wa jioni haikuwa rafiki, hivyo tumejitahidi na tukashindwa kupata matokeo."

“Simba wanapaswa wapewe pongezi kwa kutumia vizuri upungufu wetu ila hatujapoteza na bado tuna kazi mbele, hatujakata tamaa tunaenda kujipanga kwa dakika 90 zijazo," Mosimane.

Mechi inayofuata ya Simba itachezwa kati ya Machi 5 na 6, mwaka huu, jijini Khartoum dhidi ya wenyeji Al Merrikh na baadaye itarudi nyumbani kuwasubiri Wasudan hao ambao wanaburuza mkia.

Wakati huo huo, shangwe zilizoonyeshwa na mashabiki wa Simba zimewavutia mabosi wa Mamelodi Sundowns ambao wameomba sapoti katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Habari Kubwa