Simba ubingwa, Zahera atoa kilio

27May 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Simba ubingwa, Zahera atoa kilio
  • ***Morogoro hapatotosha ikiivaa Mtibwa kesho, Aussems aongezwa mwaka, wachezaji Yanga wazidi kumchanganya...

WAKATI kikosi kamili cha Simba kikitarajia kutua mkoani Morogoro leo kubabidhiwa ubingwa wao, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, analalamika kuwakosa baadhi ya wachezaji wake mazoezini ili kujiandaa na mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu.

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Simba watafunga pazia la ligi hiyo ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Yanga na Azam FC zenyewe zitakutana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Zahera alisema jana kuwa wachezaji wake nyota wameshindwa kuhudhuria katika mazoezi ya juzi na jana kutokana na kuwa wagonjwa, lakini akakasirika na kitendo cha beki wake wa kati, Kelvin Yondani kutojulikana alipo.

"Yondani si mgonjwa na wala hatuna taarifa zake, tunampigia simu hapokei na wala hatujui yupo wapi, anafanya mambo ya ovyo sana! Nimemtuma Cannavaro (Nadir Haroub) aende kwake kumwangalia halafu ataniletea  mrejesho, hapo ndipo nitajua nifanye uamuzi gani kuhusu Yondani, " alisema Zahera.

Kocha huyo aliongeza kuwa anahitaji kumaliza msimu kwa kupata ushindi licha ya kwamba tayari watani zao, Simba wameshafanikiwa kutetea ubingwa waliokuwa wanaushikilia baada ya kufikisha pointi 92 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine msimu huu.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia gazeti hili kuwa wataelekea Morogoro na wachezaji wote kwa sababu ndiko watakapopokea kikombe cha ubingwa na kuvaa medali.

Rweyemamu alisema kuwa licha ya kutetea ubingwa, wamejiandaa kupambana ili kushinda mchezo huo wa mwisho ili wapokee kombe lao kwa furaha kwa sababu hiyo ndio zawadi kubwa kwa mashabiki wao.

"Safari ya Morogoro ni kesho (leo), na mpango wetu ni kwenda na wachezaji wote, tunahitaji kwenda kumaliza msimu kwa kishindo, tunajua Mtibwa Sugar ni timu ngumu na yenye wachezaji wazoefu," aliongeza meneja huyo.

Bodi ya Ligi (TPLB), ilitangaza kuwa itawakabidhi kikombe chao cha ubingwa kesho baada ya hapo juzi kuahirisha kutokana na aliyekuwa mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kupata udhuru.

Ofisa Mtendaji wa bodi hiyo, Boniface Wambura, alisema jana kuwa sherehe zote sasa zitafanyika Morogoro na wanaamini mambo yatakwenda vema kama walivyotarajia.

Kutokana na kutwaa ubingwa huo, Simba ambayo inafundishwa na Mbelgiji Patrick Aussems ambaye jana amesaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi wa kuendelea kuinoa klabu hiyo, mwakani itaiongoza tena timu hiyo kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati KMKM yenyewe itapeperusha bendera hiyo kwa upande wa Zanzibar.

Habari Kubwa