Simba uwanjani Dodoma leo

11Mar 2017
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba uwanjani Dodoma leo

KATIKA kujiimarisha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, vinara wa ligi hiyo, Simba leo watashuka kuwakabili Polisi Dodoma katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliomba mechi hiyo ya kirafiki ili kuwafanya wachezaji wake waendelee kuwa na 'joto' la mashindano wakati michezo ya Ligi Kuu Bara imesimama kwa muda.

Omog alisema kuwa kwake mechi ya leo anaipa uzito kwa sababu anataka kuona wachezaji wake wanashinda na kuwafurahisha pia mashabiki wa timu hiyo wa mkoa huo.

"Ni mechi ya kirafiki, lakini kiufundi tunaiangalia kwa jicho lile lile linalofanana na pale tunapocheza na Yanga, hatutaki kupoteza mechi yoyote kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu huu," alisema Omog.

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC aliongeza kuwa licha ya kuwa na majeruhi, amewataka wachezaji watakaopata nafasi ya kucheza kuonyesha uwezo wao na kuwania namba katika kikosi cha kwanza.

"Hii ni timu, mchezaji atakayecheza vizuri atanishawishi kumpanga katika kikosi cha kwanza au kusubiri kwenye orodha ya wachezaji 18, kuna baadhi ni wazuri wakianza au wakiingia baada ya kuwasoma wapinzani," Omog aliongeza.

Baada ya mechi ya leo, Simba inatarajiwa kuelekea Tabora kucheza mechi nyingine ya kirafiki huku Jumapili ikitua Arusha kuwakabili wenyeji Madini FC katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA.

Habari Kubwa