Simba vitani leo bila Bocco

26Feb 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba vitani leo bila Bocco

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba wanatarajia kushuka dimbani leo kuikaribisha Mbao FC kutoka Mwanza katika mechi ya ligi hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam bila ya huduma ya mshambuliaji wake aliye katika kiwango cha juu, John Bocco.

Masoud Djuma.

Mshambuliaji huyo aliyetua Simba akitokea Azam FC aliumia katika mchezo wa raundi ya 19 dhidi ya Mwadui FC iliyofanyika Februari 15 mwaka huu na kumfanya akose pia mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmarie Nationale FC ya Djibouti bado ni mgonjwa.

Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya sare ya mabao 2-2 waliyoipata katika mechi ya kwanza dhidi ya Mbao kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza huku wakipata matokeo kama hayo walipokuwa ugenini Shinyanga wakicheza na Mwadui FC kabla ya kusafiri kwenda Djibouti.

Kocha Msaidizi wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya Michezo, SportPesa, Masoud Djuma, alisema kuwa wataingia uwanjani kwa ajili ya kuendelea na kazi moja ya kusaka pointi tatu ambazo zitawaongezea nguvu ya kuusaka ubingwa wa ligi.

Djuma alisema hakuna mechi rahisi kwenye ligi au mashindano ya kimataifa na wamewaandaa wachezaji wao kupambana kuanzia dakika ya kwanza hadi filimbi ya mwisho.

"Tunaingia kwa ajili ya kusaka ushindi, hakuna mechi nyepesi, hatuwezi kubweteka, tunajua Mbao ni wazuri na ni moja ya timu ambazo zinapata matokeo mazuri dhidi ya Simba au Yanga, kwa kifupi itakuwa mechi ngumu na yenye ushindani," alisema Djuma.

Naye Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema kuwa Bocco bado ni mgonjwa na hataweza kucheza katika mechi ya leo.

"Bado mgonjwa, ila siwezi kusema atarejea lini uwanjani, daktari anaendelea kupambana kuhakikisha anarejea mapema kuungana na wenzake kwenye vita ya kuwania ubingwa," alisema mratibu huyo.

Simba yenye pointi 42 inaongoza ligi ikifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga ambao wamejikusanyia pointi 37 wakati mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Azam FC wao wana pointi 35 na Singida United ya Singida inakamilisha "Top 4" kwa kuwa na pointi 34.  

 

Habari Kubwa