Simba wagongwa

18Jan 2022
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba wagongwa
  • ***Gonjwa la kukosa penalti lazidi kuwa sugu, safari hii lahamia kwa Mugalu, lakini...

HUKU ikikosa mkwaju wa penalti dakika mbili baada ya mapumziko, timu ya Simba imepoteza mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kukubali kupigwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

'Wekundu wa Msimbazi' hao wamepoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, baada ya kucheza mechi 10 na kuwaacha watani zao wa jadi, Yanga ambao ndiyo timu pekee iliyosalia haijapoteza mchezo wowote hadi sasa.

Licha ya Mbeya City kucheza pungufu kwa dakika 47, baada ya mchezaji wake Mpoki Mwakinyuke kuzawadiwa kadi nyekundu kwa kumchezea madhambi Chris Mugalu, waliweza kuizua Simba ambayo kipindi cha pili iliamua kucheza na mastraika wake wote watatu, Mugalu, Meddie Kagere na John Bocco.

Ugonjwa wa Simba ulikuwa ni ule ule wa kukosa penalti, safari hii, Mugalu akiikosesha timu yake kupata angalau sare dakika ya 47, alipogongesha nguzo ya pembeni, uliporejea ulimkuta Bocco akiwa kwenye nafasi nzuri ya kuupiga moja kwa moja, lakini alitaka kuuvuta na kuuweka vizuri, hali iliyompa nafasi kipa Deogratius Munishi 'Dida' kuudaka.

Inakuwa ni penalti ya nne kukosa kati ya tano kwenye Ligi Kuu. Wengine waliokosa ni Bocco kwenye mechi dhidi ya Biashara United, Erasto Nyoni akikosa ilipocheza dhidi ya Ruvu Shooting na Rally Bwalya aliyekosa dhidi ya Azam FC, lakini Bwalya ndiye mchezaji pekee aliyefunga penalti akiipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mbeya City ndiyo walianza mechi hiyo kwa kuchangamka zaidi kuliko Simba, kwani dakika ya nne tu Juma Luzio nusura awafunge waajiri wake wa zamani, aliposahauliwa na mabeki wa Simba na kubaki yeye na kipa Aishi Manula, lakini shuti lake la mguu wa kulia lilipaa juu.

Dakika nne baadaye, Samson Madeleke akiwa umbali wa mita zipatazo 35, aliachia kombora kali, lililomlazimu Manula kuruka juu na kuupangua, akiiweka Simba salama.

Ndipo dakika ya 19, straika mkongwe ambaye aliwahi pia kuichezea Yanga, Paul Nonga aliiandika Mbeya City bao, baada ya mpira mrefu uliopigwa nyuma, akawazidi mbio mabeki wa Simba ambao walikosa umakini na kuukwamisha wavuni.
Hadi wakati huo Simba ilikuwa haijafanya shambulio lolote la maana kwenye lango la wenyeji wao.

Bao hilo lilionekana kuwazindua wachezaji wa Simba na kujiona sasa wapo uwanjani, wakafanya shambulizi la kwanza dakika ya 23, Bernard Morrison alipoingia ndani ya eneo la hatari na kupiga krosi kwa Mzamiru Yasssin ambaye shuti lake liliwababatiza mabeki wa Mbeya City na kurejea uwanjani.

Mzamiru, nusura afunge bao baada ya kuufuma mpira uliorudishwa na mabeki wa Mbeya City kipa Deogratius Munishi 'Dida' akiwa ametoka golini, lakini waliuwahi na kuufagia kabla haujaingia wavuni.

Kibu Denis ambaye aliwasumbua mno mabeki wa Mbeya City alikosa bao, baada ya kuunganisha mpira wa krosi kutoka kwa Morrison, ukatoka sentimeta chache nje ya lango.

Kipindi cha pili baada ya Mpoki kupewa kadi nyekundu, Mbeya City ililazimika kucheza kwa kuzuia zaidi na kufanya kazi kubwa kuwazuia wachezaji wa Simba waliokuwa wakishambulia mfululizo.

Papara na presha ya wachezaji wa Simba ziliwafanya kukosa mabao dakika ya 58, Sadio Kanoute akipiga shuti nje, huku kichwa alichopiga Bocco dakika ya 70 kiliokolewa kwa ustadi na kipa Dida aliyewahi kuidakia timu hiyo.

Pamoja na mabadiliko ya pande zote, lakini hayakubadili matokeo ya mchezo huo.

Ni matokeo yanayoifanya Simba kuendelea kuwa nafasi ya pili, lakini ikisalia na pointi zile zile 24, saba pungufu ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga yenye pointi 32, lakini ikiwa na mechi moja mbele.

Kwa ushindi huo, Mbeya City imepanda hadi kwenye nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 19.

Habari Kubwa