Simba waifanyia kazi ripoti ya Gomes

29Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba waifanyia kazi ripoti ya Gomes

UONGOZI wa Simba umesema baada ya mapumziko ya wiki mbili kwa wachezaji wao wanatarajia kurejea kwa kishindo kwa kusajili kikosi imara 'Unbeaten' kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah, 'Try Again' alisema wanaendelea vizuri na mipango yao ya maboresho ya kikosi ikiwamo kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Alisema viongozi wana uhakika na wachokifanya, ikiwamo kuwa makini katika usajili wao kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi imara zaidi.

"Kila kitu kinaenda vizuri, Wanasimba wanatakiwa kutulia na kusubiri waone kazi yetu inayofanywa na viongozi wao, baada ya kupokea ripoti ya Kocha Gomes (Didier) na kufanyia kazi mapendekezo yake ikiwamo usajili wa wachezaji wenye kiwango kizuri na kuwa na kikosi imara ambacho ni 'Unbeaten'," alisema Try Again.

"Tumejipanga vizuri katika usajili wetu, mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba wanatakiwa kuwa watulivu kwa sababu wanafanya maboresho kwenye mapungufu yao kulingana na mahitaji."

Alisema watafanya marekebisho madogo kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi kuelekea katika mipango yao ya msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na kutaka kufanya vizuri na kutawala soka la Afrika.