Simba wasaka heshima Songea

11May 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Simba wasaka heshima Songea

IKIWA haina nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani, timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam inatarajia kuwakabili wenyeji Majimaji katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaofanyika leo mjini Songea mkoani Ruvuma.

mashabiki wa simba.

Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 6-1 iliyopata katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Oktoba 31 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Nyota wake wawili wa kigeni kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast na kiungo mkabaji Mzimbabwe Justice Majabvi waliungana na timu hiyo jana jioni baada ya madai yao ya mishahara kulipwa huku Hamisi Kiiza, Brian Majwega na Juuko Murshid wakibaki Dar es Salaam.

Kocha wa mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja aliliambia gazeti hili kuwa watashuka uwanjani kusaka 'heshima' baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

"Tutaingia uwanjani kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi, hata kama tumepoteza nafasi ya ubingwa, hatuoni sababu ya kupoteza mechi hii, tunasaka heshima," alisema Mayanja.

Alisema licha ya kikosi chake kuwa na changamoto mbalimbali, bado anawaamini wachezaji wake waliobakia watapambana ili kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo.

Yanga ndiyo mabingwa wa ligi hiyo na katika msimamo wa ligi wanafuatiwa na Azam FC yenye pointi 60 wakati Simba iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 58 huku Majimaji inayonolewa na Kally Ongala ipo katika nafasi ya 10 baada ya kujikusanyia pointi 33.

Habari Kubwa