Simba watanguliza "mashushushu" Mbeya

03Nov 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Simba watanguliza "mashushushu" Mbeya

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kikosi chake hicho kitatua jijini Mbeya kikifahamu wazi kuwa wapinzani wao Mbeya City ni "imara" na wanatakiwa kutumia nguvu za ziada ili kuhakikisha wanapata pointi zote tatu.

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog.

Mbeya City inatarajia kuwakaribisha vinara Simba katika mechi ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu Sokoine jijini Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog, alisema kuwa mechi zote za ligi kwa Simba ni sawa na fainali, lakini za ugenini huwa ni zaidi kutokana na kubadilisha mazingira ya uwanja.

Omog alisema kuwa bado amewaandaa wachezaji wake kuendeleza kasi waliyoionyesha kwenye mechi zilizopita licha ya kupata matokeo ya sare.

"Hakuna mechi rahisi, hakuna timu ndogo, tunacheza ligi moja na hivyo tunatakiwa kupambana katika kila mchezo ili kufikia malengo, lengo letu kubwa ni kutwaa ubingwa na ikiwezekana iwe mapema kabla ya mechi ya mwisho ya msimu," alisema Omog.

Naye Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema kuwa kikosi cha Simba kitawasili Mbeya leo na kuweka kambi nje ya jiji hilo ili kuendelea na mazoezi kabla ya kuwavaa wenyeji wao.

"Mimi niko Mbeya tayari kwa ajili ya kuweka mambo sawa, tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri mechi yetu ya Jumapili na ile ya Prisons itakayofanyika Novemba 18, tunajua Mbeya ni pagumu, lakini tutapambana," alisema mratibu huyo.

Aliwataja wachezaji ambao Simba itaendelea kuwakosa kutokana na kuwa majeruhi ni pamoja na Salim Mbonde, Saidi Mohammed na Shomary Kapombe, ambaye bado anaendelea na kliniki maalumu.

Ili kujiandaa na mchezo huo, kikosi cha Mbeya City kilichoko chini ya kocha wake raia wa Burundi, Ramadhani Nsanzurwino, kiliingia kambi juzi huku wachezaji wake ambao ni majeruhi ni Haruna Shamte na John Kabanda.

Habari Kubwa