Simba yaahidi furaha Lindi

08Jul 2020
Somoe Ng'itu
Lindi
Nipashe
Simba yaahidi furaha Lindi
  • Ni katika kunogesha sherehe za ubingwa, huku Yanga ikijiuliza tena kwa Kagera Sugar Kaitaba...

VIWANJA tisa vya hapa nchini vinatarajia kuwa na hekaheka za mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini macho yote yanatarajiwa kuelekezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa ambapo mabingwa wa msimu huu 2019/20, Simba watakapovaana na wenyeji wao, Namungo FC.

Tayari Simba ilishatangazwa kuwa mabingwa kwa msimu wa tatu mfululizo na leo baada ya mechi hiyo watakabidhiwa kombe lao ambalo watalichukua moja kwa moja.

Simba itashuka katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha bao 1-0 walichopokea kutoka kwa Kagera Sugar wakati wakikabidhiwa kombe la msimu uliopita, wakiwa mbele ya Rais, John Magufuli.

Namungo FC ambao wanashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza wataingia dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa magoli 3-2 na mabingwa hao walipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza jijini, Dar es Salaam, lakini kikosi hicho cha Kocha Mkuu, Hitimana Thiery, hakijapoteza mechi yoyote, kati ya michezo 17 iliyopita ya ligi hiyo pamoja na mashindano ya Kombe la FA.

Kocha Mkuu wa Simba, SvenĀ  Vandenbroeck, ameliambia gazeti hili kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na wamejipanga kupata ushindi ili kutoharibu sherehe za kukabidhiwa kikombe.

Sven alisema kila mchezaji yuko tayari na amewataka kuongeza umakini ili watimize malengo yao ya kufanya vizuri zaidi msimu huu.

"Tuko tayari kwa mechi, najua haitakuwa rahisi kutokana na wenyeji kuwa na timu nzuri pia, wanacheza kwa kasi na wanauzoefu pia na mechi kubwa, wana rekodi nzuri kama ambavyo sisi tunahitaji kuweka rekodi yetu, natumaini itakuwa mechi yenye kuvutia pia," alisema Mbelgiji huyo.

Nahodha wa timu hiyo, John Bocco alisema kila mechi kwao ni muhimu na wataingia uwanjani kusaka ushindi bila kujali wameshakamilisha hesabu za ubingwa.

"Tuko imara na tayari kwa mechi, hakuna mechi rahisi katika ligi, sisi ni mabingwa, lakini haimaanishi tutaingia uwanjani kukamilisha ratiba, tunataka ushindi wa kupokelea kikombe," Bocco alisema.

Luc Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga, aliliambia gazeti hili safari na malengo yake ni kuona wanamaliza Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa katika nafasi ya pili na hilo litawezekana kama watashinda michezo yote mitano iliyobaki.

Kocha huyo alisema wanahitaji kupata heshima hiyo baada ya kushindwa kutwaa taji, huku wakijiandaa kuwaondoa watani zao kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA hapo Jumapili.

"Nimeongea na wachezaji wangu kuhusu mechi hii, nimewaambia tunatakiwa kuwafunga Kagera Sugar halafu ndio kuifikiria zaidi Simba, ingawa haitakuwa kazi rahisi, tumekutana mara nyingi na wamekuwa wakitusumbua, hata kesho (leo), hatutakuwa na kazi rahisi, tunatakiwa kupambana," Eymael alisema.

Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo Mghana, Bernard Morrison atakuwapo katika mchezo huo baada ya kuikosa mechi iliyopita dhidi ya Biashara United ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema anaijua vema Yanga na kama mchezo utachezwa kwa haki, pointi tatu zitabaki Bukoba.

"Nawajua walivyo, hawanisumbui kama tunacheza nao bila nguvu ya ziada, naahidi vijana wangu wataendelea kuonyesha soka la kuvutia na ushindani, subirini muda utaongea," Maxime alisema.

Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Azam dhidi ya Mwadui FC, Mbao vs Mtibwa Sugar, Ndanda vs JKT Tanzania, Alliance vs Lipuli, Mbeya City vs Polisi Tanzania, Biashara United vs Ruvu Shooting na KMC watawakaribisha Singida United.

Raundi ya 34 ya ligi hiyo itakamilika kesho kwa Tanzania Prisons kuwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya

Habari Kubwa