Simba yabanwa Mapinduzi Cup

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba yabanwa Mapinduzi Cup

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wameanza michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kubanwa mbavu na Mwenge FC ya Pemba baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Amaan jana.

kikosi cha simba.

Simba ambao waliingia Zanzibar juzi mchana wakitokea Mtwara kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC  ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na siku iliyofuata kuunganisha safari ya Zanzibar, walikuwa wa kwanza kupata bao la mapema dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa beki Jamal Mwambeleko ambaye kwenye mchezo wa jana alichezeshwa kama winga.

Mwambeleko, alifunga bao hilo akiunganisha kwa kichwa krosi safi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala' ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 26 pekee, ambapo katika dakika ya 28, Mwenge walisawazisha kupitia kwa Humoud Abrahaman aliyetumia makosa ya mabeki wa Simba waliochelewa kuondoa mpira wa hatari langoni mwao.

Simba ambayo iliwaanzisha wachezaji wengi wa kikosi cha pili ambao hawachezi mara kwa mara kwenye ligi, iliendelea kulisakama lango la Mwenge, lakini safu ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na Juma Liuzio na Moses Kitandu ilikosa umakini kwenye umaliziaji.

Kipindi cha pili, kocha wa Simba, Masoud Djuma, alifanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji watatu kwa mpigo, Kitandu, Liuzio na Mwambeleko na nafasi zao kuchukuliwa na John Bocco, Shiza Kichuya na Nicolaus Gyan.

Mabadiliko hayo yaliiongezea Simba nguvu na kasi na kuanza kuliandama mfululizo lango la Mwenge, lakini bado umakini kwenye umaliziaji haukuwa mzuri.

Simba walikosa mabao ya wazi kipindi cha pili kupitia kwa Bocco na Gyan baada ya kuunganisha vibaya krosi za Tshabalala.

Katika mchezo wa awali uliochezwa saa 8:00 mchana, Singida United waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Zimamoto.