Simba yacharuka Afrika

29Nov 2018
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yacharuka Afrika
  • ***Yawashangaza Waswazi dakika za mwisho, yaipiga 4-1…

MAGOLI mawili ya nahodha wake John Bocco, Meddie Kagere na Clatus Chama, jana yaliishangaza Mbabane Swallows ya Swaziland baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa.

Baada ya kuikosa michuano hiyo kwa miaka mitano, huku mara ya mwisho ikitolewa na Recreativo de Libolo ya Angola, jana ilionyesha kuwa imepania kufanya vyema mwaka huu.

Iliwachukua wenyeji waliokuwa wakicheza dakika saba tu kuandikisha bao lake la kwanza likifungwa na Bocco, akimalizia krosi safi ya chini iliyopigwa na Nicolaus Gyan.

Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika 17 tu kabla ya wageni kusawazisha kwa shuti kali lililopigwa na Guivane Nzambe, lililomshinda kipa Aishi Manula na kujaa wavuni.

Nzambe aliutumia vyema mpira uliokolewa na mabeki wa Simba na kumfikia.

Kuingia kwa bao hilo kuwaliwafanya Simba kuanza kusaka bao linguine, lakini Mbabane walionekana kuwabana wapinzani wao hao, hata hivyo Simba ilipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Bocco dakika ya 32 baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari na golikipa wa Mbabane Swallows.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, licha ya Simba kufanya mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la wapinzani, walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko ambayo kwa kiasi kikubwa yaliisaidia kubadilisha mfumo wa uchezaji na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka yaliyoifanya timu hiyo kujiweka nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Okwi ambaye hakuwa kwenye kiwango chake cha kawaida, alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Shiza Kichuya, huku Bocco akitoka nje na nafasi kuchukuliwa na Hassan Dilunga.

Ilikuwa ni dakika ya 83 wakati Kagere alipofunga bao la tatu, kuufuata mpira mrefu uliorudishwa na beki wa Mbabane na kipa wake kushindwa kuzuia vizuri, badala yake aliteleza na mfungaji akiwa amefika kwa wakati na kuujaza wavuni.

Wakati kila mtu akiamini kuwa mechi inamalizika kwa matokeo hayo, Cletus Chama, aliipatia Simba bao la nne dakika ya 90, kufuatia kazi nzuri ya mtokea benchi, Dilunga aliyewaadaa mabeki wa Mababane kabla ya kumpa pasi safi mfungaji.

Ili kuingia hatua inayofuata ya michuano hiyo, Simba sasa inatakiwa ushindi au sare ya aina yoyote, lakini isiruhusu kufungwa mabao 3-0 kwenye mechi ya marudiano.

Mechi ya jana ilishuhudiwa na mmiliki wa asilimia 49 ya Simba, mfanyabiashara na mwanachama wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, ambaye alijikuta akisimama na kupiga makofi wakati Chama akifunga bao la nne.

Habari Kubwa