Simba yafunguka adhabu moto CAF

18May 2022
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba yafunguka adhabu moto CAF

WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakishuka dimbani leo kuvaana na Azam FC, wameomba radhi kwa wanachama na mashabiki wake, baada ya kupatikana na kosa lililoitwa 'mila hatarishi'...

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.

....na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa kuwasha moto uwanjani kwenye mechi robo fainali ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, uliochezwa Aprili 24, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema halikuwa tukio zuri, hivyo wanaomba radhi wanachama na mashabiki wa Simba waliojisikia unyonge au kuhisi kukwazika na jambo hilo, akiahidi halitojirudia tena.

Meneja Habari na Mawasiliano huyo alisema hayo jana, baada ya juzi jioni CAF kuipiga faini ya dola 10,000 sawa na Sh. milioni 23 za Tanzania kwa kile ilichokiita kufanya 'mila hatarishi' uwanjani kwa kuwasha moto katikati ya uwanja kwenye mechi dhidi ya Orlandi Pitares, iliyopigwa Uwanja wa Orlando, Afrika Kusini na Simba kutolewa kwa mikwaju 4-3 ya penalti, baada ya sare ya bao 1-0, kila timu ikishinda nyumbani.

"Hiyo haina mjadala, adhabu imetoka CAF na iliyobaki ni kuitekeleza, ilitoka jana (juzi) jioni wakati ofisi zimefungwa, leo (jana), tunakwenda kujadili na kufanya maamuzi, kama ni kukata rufani au kulipa na baada ya hapo tutatoa maamuzi," alisema Ahmed.

Kuelekea mechi ya leo dhidi ya Azam, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, amesema mchezo huo utakuwa mzuri kutokana na wachezaji aliokuwa nao na aina ya uwanja ambao wanaenda kuutumia.

Alisema kikosi chake kipo tayari kuhakikisha kinapambana kutafuta pointi tatu ambazo zitawaweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.

“Azam FC ina wachezaji wazuri, lakini hata benchi la ufundi lao liko vizuri tunaenda kupambana kuhakikisha tunapata matokeo chanya ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wetu,” alisema Pablo.

Imeandaliwa na Adam Fungamwango na Saada Akida

Habari Kubwa