Simba yaifyeka Coastal Union

20Mar 2016
Sanula Athanas
Tanga
Nipashe Jumapili
Simba yaifyeka Coastal Union

SIMBA jana ilivunja mwiko wa kutoifunga Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga tangu mwaka 2011, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa bao la kila kipindi kutoka kwa Danny Lyanga na Hamisi Kiiza.

kocha wa simba jackson mayanga.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa imefikisha pointi 57, ikizizidi Yanga na Azam FC kwa pointi saba, huku pia timu hiyo ya Msimbazi ikiwa mbele kwa michezo mitatu.

Yanga na Azam zina ratiba za mechi za kimataifa wikiendi hii. Jangwani walishuka dimbani jana na Azam watacheza leo.
Baada ya kuzitia adabu timu Yanga na Azam kwenye uwanja huo, Coastal Union walishindwa kwenda sambamba na muziki wa Simba.

Matokeo hayo yanawaacha vijana hao wa Tanga katika nafasi ngumu ya kujaribu kujinusuru na janga la kushuka daraja kutokana na kuburuza mkia wakiwa na pointi 19, moja juu ya African Sports pia kutoka Tanga.

Katika mechi hiyo kali iliyojaa ushindani wa kila aina, Simba waliostahili ushindi wangeweza kupata mabao mengi kama washambuliaji wake wangekuwa makini.

Hata hivyo, dakika ya 39, mshambuliaji aliyesajiliwa na Simba wakati wa dirisha dogo, Danny Lyanga aliifungia Simba bao la kwanza kwa kichwa, likiwa la nne kwake msimu huu, akimalizia krosi iliyochongwa na beki wa kushoto, Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Hata hivyo, Lyanga hakushangilia bao hilo kama ilivyo kawaida, pengine kutokana na kukuzwa na timu hiyo ya Tanga kabla ya kuwika kwenye timu kubwa.

Wekundu hao wa Msimbazi waliendelea kukandamiza mashambulizi langoni mwa Coastal Union na kufunga bao la pili kupitia Hamis Kiiza aliyemalizia krosi ya beki, Emery Nimubona.

Bao hilo lilimfanya kufikisha 19 katika mechi 24 msimu huu na kufikia rekodi ya mfungaji bora ya msimu wa 2013/14, Amiss Tambwe anayecheza Yanga.

Habari Kubwa