Simba yaing'oa Yanga kileleni

07Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Simba yaing'oa Yanga kileleni
  • Timu hiyo ya Msimbazi imefanikiwa kuifunga kwa mara ya kwanza Mbeya City FC kwenye Uwanja wa Taifa na kulipa kisasi cha kupigwa 'nje-ndani' msimu uliopita.

MABAO mawili ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Danny Lyanga na Hassan Mwasapili aliyejifunga katika dakika ya mwisho ya mchezo kwenye Uwanja wa Taifa, yalitosha kuipa Simba ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya City FC na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hassan Mwasapili wa Mbeya City akichuana na Ibrahim Ajibu wa Simba

Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo ya Msimbazi ifikishe pointi 48 baada ya mechi 21, hivyo kuwang'oa Wanajangwani kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya wiki mbili tangu walipoichapa timu hiyo ya Msimbazi mabao 2-0.

Ushindi wa jana pia ulimaanisha kikosi cha mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara kimeshinda mechi zote mbili dhidi ya City msimu huu na kulipa kisasi cha kupigwa 'nje-ndani' msimu uliopita, kikishinda 1-0 jijini Mbeya Oktoba 17 mwaka jana katika duru la kwanza.

Hata hivyo, hakikuwa kazi rahisi kwa kikosi cha kocha mkuu wa muda Mganda Jackson Mayanja kushinda mechi ya jana kutokana na mbinu ya mchezo wa kuotea ambao Ciy iliitumia kwa nyota wa Simba.

Mchezo huo ulionekana kumshinda kinara wa mabao msimu huu, Hamisi Kiiza ambaye alicheza dakika 59 za kwanza na kulazimika kumpisha Awadh Juma.

Simba walisubiri hadi dakika ya 75 kupata bao la kwanza kupitia kwa Lyanga aliyemalizia mpira wa shuti kali la kiungo mtokea benchi, Awadh lililotemwa na kipa Hannington Kalyesabula. Baada ya bao hilo, Mbeya City walipiga kambi kwenye lango la Simba wakisaka kusawazisha kupitia kwa washambuliaji wao waliotokea benchi,

Themi Felx na Ramadhani Chombo 'Redondo', lakini safu ya ulinzi ya Simba chini Mganda Juuko Murshid na Novaty Lufunga ilisimama imara.

Wakati kibao cha refa wa mezani, Israel Nkongo kikisomeka dakika moja ya majeruhi katika dakika ya 90, Simba walifanya shambulizi la kushtukiza wakipita kusini magharibi mwa Uwanja wa Taifa na kufanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa beki wa pembeni kushoto, Mwasapili aliyejifunga wakati akijaribu kuosha mpira wa shuti la ndani ya sita lililopigwa na staika Ibrahim Ajibu na kuibabatiza mikono ya kipa Kalyesabula.

Mashabulizi hatari zaidi ya City jana yalikuwa katika dakika za 24 na 61, lakini shuti la Ditram Nchimbi halikulenga lango kabla ya mpira wa kichwa cha ndani ya sita cha mpigapenalti mkuu wa timu hiyo, Alpha kupita pembeni kidogo mwa nguzo ya lango la kusini mwa Uwanja wa Taifa.

Licha ya kupoteza mechi hiyo, kocha mkuu wa City, Mmalawi Kinnah Phiri, aliwapongeza nyota wake kwa kufuata kwa kiasi kikubwa maelekezo aliyokuwa amewapa akidai kuwa wamefungwa kwa sababu hawakuwa na bahati ya kufunga magoli.

Simba na City zimekutana mara sita katika ligi ya Bara tangu timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ianze kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2013/14 iliomaliza nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Azam FC na Yanga (nafasi ya pili) ikitoka sare katika mechi zote mbili dhidi ya Wanamsimbazi.

Habari Kubwa