Simba yaipa nafasi Yanga

14May 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba yaipa nafasi Yanga
  • ***Azam yaitibulia, ubingwa sasa shughuli pevu, vijana wa Zahera kurejea kileleni leo endapo...

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameshindwa kuendeleza kipigo dhidi ya Azam FC kwenye mechi yao ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo baada ya kulazimishwa sare tasa katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana-

na hivyo kutoa nafasi kwa watani zao, Yanga kurejea kileleni leo.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa uwanjani hapo, mwezi uliopita, Simba ilishinda 3-1, matokeo ambayo yaliukera uongozi wa Azam na hivyo kuamua kumtimua Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm pamoja na msaidizi wake, Juma Mwambusi.

Kwa matokeo hayo ya jana, yanaifanya Simba kufikisha pointi 82 baada ya mechi 33, wakati Yanga yenye alama 80 zilizotokana na michezo 35, inaweza kurejea kileleni mwa ligi hiyo endapo itaibuka na ushindi dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Uhuru leo.

Lakini huenda ikakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Ruvu Shooting inayokamata nafasi ya 13 ikiwa na pointi 42, kwani nayo inahitaji pointi tatu ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja, au kwenda kwenye mechi za mtoano  'play off.'

Sare hiyo kwa Simba imekuja wakati ikitoka kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi iliyopita ambayo ilipigwa uwanjani hapo.

Hata hivyo, makocha wa timu hizo wameeleza kuwapo changamoto ya maji kwenye uwanja ambayo yametuama na kusababisha mpira wakati mwingine kukwama kutembea na kupoteza ladha ya mchezo.

Katika mchezo huo, timu zote mbili zilifanya mashambulizi kwa kupokezana, Simba wakikosa bao kipindi cha kwanza, baada ya Emmanuel Okwi kuunganisha krosi ya Nicolaus Gyan, huku Claotus Chama akigongesha mlingoti wa goli baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Azam.

Azam ambayo matokeo hayo yanaifanya kufikisha alama 69 baada ya mechi 36, nayo ilipata nafasi nzuri kipindi cha kwanza kupitia kwa Donald Ngoma, aliposhindwa kuunganisha vizuri krosi kutoka kwa Bruce Kangwa, huku Obrey Chirwa akimpa mikononi kipa Aishi Manula alipobaki naye ana kwa ana kipindi cha pili.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Sokoine, wenyeji Prisons walikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya KMC kwenye mechi kali ya kusisimua.

Habari Kubwa