Simba yaipiga dongo Yanga

22May 2020
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaipiga dongo Yanga

SIKU chache baada ya Yanga kutangaza kuanza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yao, watani zao, Simba wamewapongeza kwa hatua hiyo lakini wamewatupia 'dongo' kuacha kulalamika hovyo kuhusiana na matokeo ya uwanjani.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara :PICHA NA MTANDAO.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema kuwa ni jambo zuri kwa Yanga kufuata nyayo zao mfumo wa uendeshaji kuzitaka klabu nyingine kufanya mabadiliko hayo ili wasiachane mbali.

"Nawapongeza Yanga kuja huku tulipo sisi, lakini ni lazima mabadiliko yao yaende na mabadiliko ya fikra zao, waache mambo ya kulalamika hovyo wanapofanya vibaya, timu inayojiita klabu kubwa haipaswi kulalamika hovyo kwa matokeo ya uwanjani, lalamika kwa hoja na sio kila kitu kulalamika," alisema Manara.

Alisema mabadiliko hayo yatasaidia mchezo wa soka hapa nchini kuwa na ushindani na wanaamini yataongeza upinzani wao kwenye ligi na mashindano yote wanayoshiriki.

Yanga imezindua mchakato wa mfumo wa mabadiliko ya uendeshwaji ikiwa ni moja ya sera kuu iliyowaweka madarakani Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolwa na makamu wake, Frederick Mwakalebela.

Habari Kubwa