Simba yaipiga Mbao mkono

27Feb 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Simba yaipiga Mbao mkono
  • ***Moto wa Okwi haukamatiki Bara, ashindwa kumaliza mechi baada ya kuumizwa... 

MSHAMBULIAJI Emmanuel Okwi, anazidi kukimbiza kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kufunga mabao mawili katika ushindi wa magoli 5-0 dhidi ya Mbao FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabao hayo ya Okwi yanamfanya sasa kufikisha idadi ya mabao 16 wakati Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ikifikisha pointi 45 kutokana na mechi 19 walizocheza.

Mbao ilijaribu kuwabana wenyeji dakika 30 za kwanza na kumlazimisha kocha wa Simba, Pierre Leshantre, kufanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa, Said Ndemla na nafasi yake kuchukuliwa na Muzamir Yassin.

Kiungo Shiza Kichuya, alikuwa wa kwanza kuipatia Simba bao la kwanza katika dakika ya 37 akitumia vyema pasi ya Okwi.

Mbao ambao walianza mchezo huo kwa kucheza zaidi katika eneo lao huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza, walijikuta wakifungwa bao la pili katika dakika ya 41 kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa kiufundi na Okwi.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi,Erick Onoka, baada ya Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Mbao FC David Mwasa na kuifanya Simba iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Simba iliendelea kuliandama lango la Mbao na katika dakika ya 69, Okwi aliitumia vyema pasi ya Muzamir kuiandikia Simba bao la tatu huku mchezaji kiraka, Erasto Nyoni, aliipa timu yake bao la nne kwa mpira wa faulo uliombabatiza beki wa Mbao FC na kumchanganya golikipa wao na kutinga wavuni moja kwa moja.

Simba ilipata pigo baada ya bao hilo baada ya Okwi kuumia na kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.

Mshambuliaji raia wa Ghana, Nicolaus Gyan, aliipa Simba bao la tano huku likiwa bao lake la kwanza msimu huu kwa shuti kali ndani ya "box" akiunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Muzamir baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Mbao.

Burudani kubwa kwenye mchezo wa jana ilikuwa kituko cha beki wa pembeni  wa Simba, Asante Kwasi, ambaye kila kocha wa Mbao FC alipokuwa akiwaiita wachezaji wake kwa ajili ya kuwapa maelekezo, Kwasi naye alikuwa    akikimbilia kama vile naye ni mchezaji wa Mbao na baada ya kusikiliza alikuwa akikimbia kwa wachezaji wenzake kuwaambia kile alichokisikia.

 

Habari Kubwa