Simba yaitisha African Lyon

26Feb 2021
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaitisha African Lyon

HATUTAWADHARAU! Hayo ni maneno ya mabingwa watetezi, Simba kuelekea mchezo wa mzunguko wanne wa mashindano ya Kombe la FA dhidi ya African Lyon utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo yanayochezwa kwa mfumo wa mtoano na bingwa wake hupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes aliliambia gazeti hili jana, kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi mapema na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Gomes alisema mechi zote ambazo timu yake inacheza ni sawa na fainali kwa sababu wanahitaji kukamilisha malengo waliyonayo ya kuchukua mataji.

Mfaransa huyo alisema katika soka hakuna mechi ndogo wala kubwa kwa sababu kila timu hujiandaa kupata matokeo chanya na amejiandaa kukabiliana na ushindani wowote kwenye mchezo huo.

"Kila siku tunakutana na changamoto tofauti, tumesahau matokeo ya mechi iliyopita na sasa akili yetu ni mchezo wa Kombe la FA, tunatarajia kukutana na ushindani hasa kwa sababu ni mashindano ya mtoano, tumejipanga kuendeleza kasi yetu tuliyonayo kwa sababu tunahitaji ubingwa wa michuano hii pia," Gomes alisema.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema wataingia katika mchezo huo kwa 'nguvu kubwa' kuhakikisha wanapata ushindi.

"Tumekuwa na tabia ya kupoteza mechi ndogo baada ya kumaliza mchezo dhidi ya timu kubwa, nimeongea na Matola (Selemani- Kocha Msaidizi) kwa ajili ya kuongeza msisitizo, mimi kwangu ni bora kufungwa 2-0 na Al Ahly, lakini sio African Lyon, tutaingia kwa nguvu ile ile tuliyoishia nayo," Manara alisema.

Aliongeza msimu huu Simba imejipanga kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini lengo kuu ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Naye Mmiliki wa African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Rahim Zamunda alisema kikosi chake kiko imara na kinaamini kitapata matokeo chanya dhidi ya mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo.

"Hatuiogopi wala kuihofia Simba, sisi tuko imara na tayari kwa mchezo wa kesho, tunauwezo ndani na nje ya uwanja, walipo wao tulishapita zamani," Zamunda alitamba.

Tayari Kagera Sugar ya Bukoba iliyowafunga Eagle Stars na wenyeji wa Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting walipata ushindi dhidi ya Mbao zimeshasonga mbele katika hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Mechi nyingine za michuano hiyo zinazotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya Arusha FC dhidi ya Mashujaa wakati Mtibwa Sugar itawakaribisha JKT Tanzania, huku Yanga ikiwaalika Kengold FC kutoka jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Uhuru.

Habari Kubwa