Simba yaiwahi TP Mazembe kwa Tshabalala

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaiwahi TP Mazembe kwa Tshabalala

WAKATI ikielezwa vigogo wa soka wa TP Mazembe ya DR Congo wapo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Simba kuhusu uwezekano wa kumnasa beki wao wa pembeni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’-

Mohammed Hussein ‘Tshabalala.

-ama ukipenda mwite 'Zimbwe Junior', nahodha huyo msaidizi amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuwatumikia mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika.

Tshabalala ambaye yupo na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ('Taifa Stars') kilichopo Cairo, Misri kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), ameelezwa alitia saini mkataba huo kabla ya kuondoka nchini Juni 7, mwaka huu, lakini jana ndiyo klabu yake ya Simba imeuanika rasmi.

Kwa mantiki hiyo, Tshabalala sasa anaungana na nahodha mkuu, John Bocco, kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, kiungo Jonas Mkude na mshambuliaji Meddie Kagere raia wa Rwanda kwenye orodha ya wachezaji ambao wameongeza mikataba yao na Simba.

Aidha, Tshabalala ambaye ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiwezesha klabu hiyo kufika robo fainali kabla ya kutolewa na TP Mazembe msimu uliomalizika, imefahamika kwamba kwa sasa anawindwa na miamba hiyo ya DR Congo.

“Ni kweli wanamhitaji Tshabalala pamoja na Fei Toto (Feisal Salum wa Yanga) na straika Kinda wa Serengeti Boys, Kelvin John ‘Mbappe',” kilieleza chanzo chetu jana.

Habari Kubwa