Simba yaizidi ujanja Yanga

14Jun 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaizidi ujanja Yanga
  • ***Yafanikiwa kumbakisha Mkude klabuni hapo na yatamba kusajili 'majembe' ya viwango...

KWA mara nyingine, mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wameendelea kuwazidi maarifa watani zao Yanga baada ya kufanikiwa kumpa mkataba mpya kiungo wake, Jonas Mkude, imefahamika.

Mkude ambaye wiki iliyopita alitemwa katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuwatumikia mabingwa hao na kuzima ndoto za Yanga ambao walikuwa wanawania saini ya kiungo huyo.

Nyota wengine wa Simba ambao tayari wameshasaini mikataba mipya ni pamoja na golikipa, Aishi Manula, Erasto Nyoni na nahodha, John Bocco, ambaye bado mkataba wake umegubikwa na utata baada ya klabu nyingine ya Afrika Kusini, Polokwane City ikisema kwamba inamtambua ni mchezaji wake halali.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema jana kuwa klabu hiyo itaendelea kuweka wazi taarifa za wachezaji wa ndani iliyowasajili kila siku, na kuanzia wiki ijayo wanawatangaza nyota wa kigeni ambao wamekamilisha mazungumzo ya kuwasajili.

"Kila siku ikifika saa 7: 00 mchana, tutakuwa tunadondosha mmoja mmoja, ila kuanzia wiki ijayo tutaanza kwa mfumo mwingine, tutawatambulisha majembe yetu ya nje," alisema Magori.

Aliongeza kuwa mwaka huu Simba itatumia zaidi ya Sh. bilioni 1.3 ambao walitumia katika msimu uliopita kwa sababu wanahitaji kupata mafanikio.

Alisema pia imeanza maandalizi kwa ajili ya 'Wiki ya Simba' itakayohitimishwa na Tamasha la Simba Day, huku ikiwapa jukumu la wasanii wanaoipenda klabu hiyo kuandaa kibao kitakachoisifia timu yao na kuchezwa katika mechi mbalimbali za timu hiyo.

 

KUACHIA NGAZI

Magori alisema kuwa anatarajia kuachia ngazi katika nafasi anayoishikilia baada ya siku 60 kumalizika.

Kiongozi huyo alisema kuwa uamuzi wa kuendelea kufanya kazi umetokana na Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kumuomba, huku wakiahidi kuanza mchakato mpya wa kuajiri watendaji wengine.

"Mimi naona ninafaa zaidi kuwa kwenye bodi, niliombwa nisaidie kwa miezi sita, kuanzia Novemba (mwaka jana), katika kipindi hiki cha mpito, na kwa sasa nimekubali kwa sababu ni kipindi cha usajili na kuandaa timu, tutatangaza nafasi hii kwa ajili na nyingine hivi karibuni," Magori alisema.

 

Habari Kubwa