Simba yakubali mambo mazito

20May 2022
Na Waandishi Wetu
DAR
Nipashe
Simba yakubali mambo mazito

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, akisema mechi yao dhidi ya Azam FC ilikuwa ngumu, mabosi wa klabu hiyo wamesema akili na nguvu zao zote ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wa Kombe la FA msimu huu.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

Pablo alisema matokeo ya sare ni ya kawaida katika mchezo wa soka lakini alibainisha mechi hiyo ya juzi ilikuwa na ushindani kwa sababu timu zote zinashabihiana uwezo na kipindi cha pili wachezaji wake walionyesha kiwango bora.

"Mchezo ulikuwa mgumu ingawa kuna nafasi ambazo tulipata tukashindwa kuzitumia, kipindi cha pili wachezaji walicheza kwa nguvu na kwa ubora wa hali ya juu," alisema Franco.

Alisema anajipanga kukutana na Geita Gold na kuongeza anaiheshimu timu hiyo kutokana na kuwa na wachezaji wazuri.

"Matokeo ya sare dhidi ya Azam sio rafiki kwetu katika mbio za kutetea ubingwa wa wa Ligi Kuu Tanzania, ni matokeo ambayo hatukusudia kupata, tulihitaji kuondoka na pointi zote tatu ambazo zingetufanya kupunguza tofauti ya pointi na wanaoongoza ligi," Pablo alisema.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema matokeo waliyopata dhidi ya Azam FC si mazuri lakini wanayaheshimu kwa sababu wachezaji wao walipambana.

“Tumekosa ushindi dhidi ya Azam FC, malengo na dhamira yetu ya ubingwa imekuwa ngumu na sasa nguvu zetu kubwa tunazielekeza katika Kombe la ASFC huku tukiendelea kupambana kutafuta pointi katika michezo sita iliyobakia katika ligi,” alisema na aliongeza;

“Kwa hali tuliyokuwapo na kwa matokeo haya malengo ya ubingwa yamezidi kuwa magumu kwa sababu ili Simba iwe bingwa lazima kushinda mechi zote na lazima wapinzani wetu wapoteze na kufanya vibaya jambo hilo ni ngumu kulingana na msimu huu kutokuwa vizuri,” alisema Ahmed Ally.

Simba inatarajia kusafiri kwenda Mwanza kuwafuata Geita Gold FC katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Imeandikwa Shufaa Lyimo na Saada Akida

Habari Kubwa