Simba yalia na ratiba, Yanga siri ya mabao

02Dec 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yalia na ratiba, Yanga siri ya mabao
  • ***Yakiri Desemba kuielemea, lakini yasema acha kazi iendelee wamalizane na Red Arrows kwanza...

WAKATI jana ikicheza mchezo wa kwanza mwezi huu, Simba imeeleza inakabiliwa na ratiba ngumu katika kipindi hiki cha Desemba, ikitakiwa kucheza michezo sita ukiwamo mmoja wa kimataifa; Kombe la Shirikisho Afrika na mmoja wa Kombe la FA, lakini upande wa watani zao, Yanga wametoa siri ya

ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza juzi.

Ratiba inayoelezwa kuwa ngumu kwa Simba ilianza jana kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold FC uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Desemba 5, itacheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows nchini Zambia.

Baada ya mchezo huo, Simba itarejea nyumbani kucheza dhidi ya Yanga Desemba 11 na kisha siku nne baadaye kuvaana na JKT Tanzania kwenye mechi ya Kombe la FA kabla ya Desemba 18 kuifuata Kagera Sugar ikiwa ni siku sita kabla ya kwenda mkoani Tabora kuvaana na KMC FC, ambayo imehamishia mechi yake hiyo Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, akizungumza na gazeti hili, alikiri kuwa ratiba imewabana, lakini hawana namna zaidi ya kupambana ili kufanya vizuri.

"Ratiba kweli imetubana kwa mwezi huu, ukiangalia baada ya mchezo wa leo (jana) tutatakiwa kusafiri kwenda Zambia kuuwahi mchezo wa marudiano dhidi ya Red Arrows, lakini ni lazima tutapambane na kujiandaa kuweza kukabiliana na ratiba hii na hapo hapo kuhakikisha timu inafanya vizuri," alisema Matola.

Aidha, alisema Kocha Mkuu, Pablo Franco, ameiona ratiba na anaandaa programu ya kukabiliana nayo huku kipaumbele chake kikiwa ni timu kufanya vizuri kwenye michezo hiyo.

Hata hivyo, wakati Simba ikieleza hayo, watani zao Yanga wamesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza juzi kwenye Uwanja wsa Sokoine jijini Mbeya ulikuwa ni mpango makakati wao kutokana na hali ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, akizungumza baada ya mechi kumalizika, alisema mchezo haukuwa rahisi hata kidogo kutokana na kwamba walicheza na timu yenye vijana wengi na wenye kujituma, hivyo mpango wao ulikuwa ni kupata mabao ya mapema ili kuufanya mchezo uwe rahisi kwao.

"Tulijua utakuwa mgumu, lakini sisi tulijiandaa kucheza na timu nzuri, yenye vijana wenye kujituma na kwa sababu kiwanja hakikuwa rafiki, tuliamua kutafuta mabao ya mapema ili kuufanya mchezo kuwa mwepesi kwetu na mgumu kwa wapinzani na ndiyo lilikuwa lengo letu kubwa," alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Alisema ushindi huo unawapa ari zaidi na kujiamini kwenda kuweka mipango ya kujiandaa na mechi inayofuata.

Yanga inajiandaa na mechi ya watani zao wa jadi, Simba, itakayochezwa Desemba 11, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mbeya Kwanza, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Haruna Hererimana, alisema wamekubali kupoteza mechi hiyo kutokana na wachezaji wake kutokuwa makini kwenye ukabaji, hasa kipindi cha kwanza.

"Tumecheza vizuri, na Yanga wamecheza vizuri, wenzetu ni wazoefu kwa hiyo walikuwa wanatumia makosa yetu kwa sababu hatukuwa makini kwenye ukabaji, tukipoteza mpira wenyewe wanapiga juu pembeni, mabeki wetu na mawinga wakawa wanachelewa kwenda kuziba nafasi mapema, hii ilitupa shida sana hasa kipindi cha kwanza, kidogo tuliziba mianya kipindi cha pili," alisema kocha huyo ambaye ni Mrundi.

Habari Kubwa