Simba yamchanganya Niyonzima

16Oct 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba yamchanganya Niyonzima

WAKATI Simba ikiendelea 'kuzidungua' timu za Ligi Kuu Tanzania Bara inazokutana nazo, Kiungo wa Kimataifa wa Yanga, Mrwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas', amesema mafanikio hayo yanawasumbua na kukiweka kikosi chao katika 'majaribu'.

Haruna Niyonzima 'Fabregas',.

Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar, Simba ilishuka dimbani mara nane, ikishinda sita na kutoka sare mbili, hivyo kujikusanyia pointi 20.

Niyonzima aliliambia Nipashe kuwa, Simba ama Yanga moja inapofanya vizuri, changamoto huongezeka upande mwingine na kwamba msimu huu kwa Yanga "imekaa vibaya".

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda 'Amavubi', alisema changamoyo hiyo itatokana na ligi kuwa na ushindani ambao umesababishwa na kila timu kufanya maandalizi bora tofauti na misimu iliyopita.

"Kiukweli ligi ni ngumu, kila timu imejipanga kufanya vizuri, ila mpaka sasa Simba wanastahili pongezi, walipofikia ni pazuri, kitu muhimu ni kila klabu kuendelea kupambana na mwisho wa msimu tutajua bingwa ni nani," alisema Niyonzima.

Aliongeza kuwa changamoto iliyopo inasaidia kuwafanya wachezaji waendelee kupambana katika kila mechi na msimu huu tayari umedhihirisha hakuna timu ndogo wala kubwa.

Kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa ligi hiyo chenye pointi 14 baada ya kushuka dimbani mara saba, leo kinatarajia kutashuka uwanjani ugenini dhidi ya mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam FC.

Habari Kubwa