Simba yampeleka Tuyisenge Yanga

27Apr 2019
Somoe Ng'itu
MUSOMA
Nipashe
Simba yampeleka Tuyisenge Yanga
  • ***Kagere, Okwi, Bocco wachangia, sasa wafuata mkali wa kutupia nje ya boksi ambaye...  

WAKATI ikiwa imeanza mazungumzo ya chini kwa chini na wachezaji wa hapa nchini kwa ajili ya kuwasajili ili kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya, uongozi wa Simba umesema nafasi ya straika wa Gor Mahia, Jacques Tuyisenge imeota mbawa.

Jacques Tuyisenge

Na kwa kauli hiyo ni wazi sasa Simba imeifungulia Yanga mlango wa kumsajili mshambuliaji huyo anayetisha kwa kutikisa nyavu Gor Mahia.

Simba na Yanga, zote zilikuwa zikiwania saini ya Tuyisenge, lakini kikosi hicho cha mtaa wa Jangwani na Twiga kilijivuta nyuma kuhofia nguvu ya fedha ya Wekundu wa Msimbazi hao na sasa inaelezwa kimeanza mbio mpya za kumsajili.

Awali kulikuwa na taarifa kuwa Simba, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilisaini mkataba wa awali na straika huyo raia wa Rwanda.

Akizungumza na gazeti hili jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema Kamati ya Usajili ya klabu hiyo imemuondoa Tuyisenge katika "rada" zake kutokana na uwezo wake kutofautiana sana na washambuliaji wao watatu tegemezi walioko sasa.

Magori alisema kuwa wameanza mipango ya kusajili mshambuliaji ambaye ana uwezo wa juu kuliko Bocco (John), Okwi (Emmanuel) au Meddie Kagere, ambao wameisaidia Simba kufika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Kiukweli Simba haina mpango na Tuyisenge, tunahitaji kuwa na mshambuliaji ambaye anawazidi kwa mbali Bocco, Okwi na Meddie, hawa wote ni wachezaji ambao wanacheza kwenye boksi, sasa anayetakiwa ni mwenye uwezo wa kufanya vitu vyote wakiwa nje ya boksi ili tufike tunakokuhitaji," alisema Magori.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kutulia kwa sababu klabu yao imejipanga kuboresha kikosi hicho ili msimu ujao iwe na mafanikio zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Hata hivyo, pia ndani ya klabu hiyo wapo wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao na bado hawajui hatima yao kutokana na kutokamilika mazungumzo kuhusu kusaini mikataba mipya.

Mchezaji mmojawapo anayetajwa kurejea katika klabu hiyo ni nahodha na mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Ibrahim Ajib.

Habari Kubwa