Simba yamwaga vifaa vya corona Muhimbili

22May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yamwaga vifaa vya corona Muhimbili

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba kwa kushirikiana na Taasisi ya Mo Dewji ya hapa nchini wamegawa vifaa na dawa mbalimbali katika Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupambana na maambukizo ya virusi vya corona (COVID 19).

Sehemu nyingine ambazo misaada hiyo imepelekwa ni Taasisi ya Mifupa ya Moi na Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Mbali na dawa hizo, pia Simba na taasisi hiyo wametengeneza mabomba kwa lengo la kusaidia wagonjwa na ndugu wanaofika kwenye hospitali hiyo kusafisha mikono na maji tiririka.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha, alisema jana kuwa klabu yao inafuraha kuona imeshiriki kupambana na ugonjwa huo kwa kusaidia jamii inayowazunguka.

Senzo alisema kwa uamuzi huo, Simba inaona faraja kushiriki katika mapambano ya ugonjwa huo ambao umetikisa dunia na kuongeza maisha yamebadilika kupitia janga hilo.

"Kwa niaba ya Simba na Bodi, ninafuraha kukabidhi vifaa hivi, ni msaada unaogusa watu, ni vizuri kuungana kushirikiana na watu, huu ni msaada wenye thamani kubwa na si suala la kuosha tu mikono," alisema Mbatha.

Alisema uamuzi wa kushiriki kutoa misaada haukuchukua mjadala na Simba inaahidi kuendelea kusaidia jamii na anaamini klabu nyingine pia zitaunga mkono zoezi hilo.

Mkuu wa Taasisi ya Mo Dewji, Barbara Gonzalez, alisema taasisi hiyo ilianza ujenzi wa mabomba ya kunawia tangu Machi, mwaka huu na wakaona si vibaya kushirikiana na Simba katika kufikia malengo yao.

Alisema bado taasisi hiyo na Simba itatoa vifaa vingine kwa ajili ya kuendelea kupambana na ugonjwa huo.

Habari Kubwa