Simba yanasa winga ‘teleza’, Okwi agoma

03Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba yanasa winga ‘teleza’, Okwi agoma
  • ***Ni aliyebeba ubingwa wa Caf na kucheza Klabu Bingwa Dunia akiwa na TP Mazembe, wamwelezea kuwa...

HUKU ikiendelea kuhaha kuipata saini ya mshambuliaji wao, Mganda Emmanuel Okwi, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wametangaza rasmi kuingia mkataba wa mwaka mmoja na winga wa Kimataifa wa DR Congo, Deo Kanda Mukok, anayeaminika ni mkali wa ‘kuteleza’ na mpira akitokea pembeni kuingia kati.

Taarifa kupitia ukurasa wa Instagram wa Simba ikiambatana na mchezaji huyo akitia saini mkataba wake akiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori, ilieleza: "Kazi ya kusajili wakali watakaohakikisha kikosi cha mabingwa kinazidi kuwa tishio kwa wapinzani inaendelea. Mshambuliaji raia wa Congo DR, Deo Kanda (29), amejiunga na mabingwa wa nchi.

"Kanda amesaini mkataba wa mwaka mmoja kukipiga Msimbazi akitokea TP Mazembe ambapo alikuwa mmoja wa wachezaji ambao waliiwezesha kushinda ubingwa wa Afrika mwaka 2009, 2010 (aliifungia bao kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Esperance) na 2013, lakini pia akiwa ameshiriki Kombe la Dunia la Klabu mwaka 2009, 2010 na 2013. #Nguvu Moja."

Kanda anakuwa mchezaji mpya wa tano wa kigeni kusainishwa kuichezea Simba msimu ujao baada ya Wabrazil watatu, mabeki Gerson Fraga Vieira kutoka ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka Klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na kiungo Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman (Al Hilal ya Sudan).

Kwa upande wa Okwi, kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Nipashe jana kutoka chanzo chetu cha uhakika ndani ya Simba, zimeeleza kuwa  suala la kuipata saini ya nyota huyo wa kimataifa wa Uganda bado kuna mvutano mkubwa kutokana na kuhitaji dau kubwa.

"Ni kweli tunahitaji saini ya Okwi lakini anahitaji dau kubwa kiasi cha Sh. milioni 115 ili asaini mkataba wa mwaka mmoja, na ametakiwa kupewa kiasi hicho lakini kwa mkataba wa miaka miwili jambo ambalo hataki kuliafiki.

"Yeye anataka kama ni miaka miwili apewe fedha zaidi ya hizo, jambo ambalo uongozi nao haujaafiki, ila subirini mambo yakiwa tayari mtafahamishwa," kilieleza chanzo chetu.

Okwi ambaye yupo nchini Misri kwenye Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2019, na akiwa ameiwezesha timu yake ya Taifa ya Uganda kutinga hatua ya 16-bora, amemaliza mkataba na Simba na hataki kuingia mkataba mpya kwa sasa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wapo Misri kwa ajili ya kuendelea kuzungumza na nyota huyo.