Simba, Yanga fainali ya kibabe Mapinduzi

13Jan 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga fainali ya kibabe Mapinduzi
  • ***Kuutapisha Uwanja wa Amaan leo, tambo zatawala kila mastaa waliobaki Dar waitwa...

MIAMBA ya Ligi Kuu Bara na watani wa jadi nchini, Simba na Yanga, leo inashuka katika dimba la Amaan visiwani hapo, kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayoikutanisha katika hatua hiyo kwa mara ya pili tangu ilipoanza kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2007.

Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kulibeba taji hilo mwaka 2007, michuano hiyo ikifanyika kwa mara ya kwanza, lakini miamba hiyo ya Bara ilikutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya fainali mwaka 2011 na Simba kulibeba taji hilo baada ya kuibuka na ushindi.

Hata hivyo, leo timu hizo zinakutana, Simba ikiwania kulitwaa kwa mara ya nne wakati Yanga ikiwania kulibeba kombe hilo kwa mara ya pili.

Simba ililitwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2008 baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwenye mechi ya fainali, kisha ikalibeba 2011 kwa kuichapa Yanga kabla ya kulinyanyua tena kombe hilo mwaka 2015 kwa kuifunga Mtibwa Sugar.

Wakati zikishuka dimbani leo, Azam FC waliotolewa na Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4 juzi baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90, wanabaki kuwa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo baada ya kulitwaa mara tano ikifuatiwa na Simba mara tatu na Mtibwa Sugar mara mbili, timu zingine zilizosalia, Yanga, Miembeni na URA, zimelibeba mara moja moja.

Hata hivyo, neno ushindi ndilo pekee linalotajwa na viongozi, makocha wa timu zote mbili, Yanga na Simba pamoja na mashabiki wa timu hizo kila mmoja akitamba timu yake kulitwaa leo katika mechi hiyo itakayopigwa majira ya saa 2:15 usiku.

Kuelekea fainali hiyo timu hizo mbili tayari zinaelezwa kuingia mchecheto wa ushindi huku zikiwaita wachezaji wao ambao walibaki jijini Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali ikiwamo mapumziko.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza nyota wa Simba akiwamo Luis Miqussoine, Clatous Chama na Rally Bwalya walitarajiwa kuungana na kikosi hicho jana jioni kwa ajili ya kuongeza nguvu katika fainali hiyo.

"Wanakuja leo (jana) kwa ndege tayari kuungana na wenzao, unajua mechi ya watani haina cha udogo wa mashindano, ukifungwa inaingia tu kwenye rekodi," alisema mtoa habari wetu, huku uongozi wa Simba ukikataa katu katu kuweka wazi kuhusu suala hilo.

Lakini kwa upande wa Yanga ambao nao kuna baadhi ya nyota akiwamo Said Ntibazonkiza, Lamine Moro nao wanaelezwa tayari wameungana na wenzao ikiwa ni pamoja na usajili mpya Dickson Job ambaye amesajiliwa juzi na Yanga akitokea Mtibwa Sugar.

Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, alisema baada ya kumaliza nusu fainali dhidi ya Azam FC wamejipanga kuwakabili Simba katika fainali hiyo, huku akieleza ataendelea kutumia wachezaji wake waliokuwapo tangu awali.

"Utakuwa mchezo wa ushindani mkubwa kwa sababu ni fainali, kila mmoja anahitaji kupata matokeo mazuri kwa upande wetu, tumejiandaa kutwaa ubingwa huo licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wangu," alisema Kaze.

Kwa upande wa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola, alisema fainali ni fainali, mchezo utakuwa wa ushindani mkubwa na anawaheshimu wapinzani wao....soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa