Simba, Yanga hakuna kulala

23May 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga hakuna kulala

VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga zinatarajia kuwaita wachezaji wake ili kuanza mazoezi ya pamoja kwa ajili ya kumalizika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2019/ 20.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli:PICHA NA MTANDAO

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema jana timu yao itaanza mazoezi ya pamoja Juni Mosi, mwaka huu chini ya Kocha Msaidizi, Boniface Mkwassa na tayari wameshawajulisha wachezaji wao.

Bumbuli alisema klabu imeshaanza kuandaa  utaratibu wa kuwarejesha wachezaji wao na makocha wao walikuwa nje ya nchi ili kuungana na wenzao mapema.

"Kwa upande wa makocha wetu wa kigeni wakiongozwa na Luc Eymael, hakuna hakika kama watarejea mapema, kwa sababu wenzetu bado viwanja vya ndege havijafunguliwa, hivyo timu itakuwa chini ya Mkwasa na makocha wengine walikuwapo," alisema Bumbuli.

Alisema ili kujikinga na corona, daktari wa timu hiyo atafuata ushauri uliotolewa na Wizara ya Afya na mamlaka husika kuwapima wachezaji kabla ya kuanza kufanya mazoezi ya pamoja.

" Leo (jana) asubuhi wataalum wa viwanja wameanza kufanya ukarabati wa Uwanja wa Chuo cha Sheria, wanaweka alama za ndani ambazo zilifutika kutokana na kutotumika kwa muda mrefu ili tuweze kuutumia kama timu," Bumbuli alisema.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kikosi chao kiko tayari kuendeleza kampeni yake ya kutetea taji hilo kama walivyofanya wakati msimu unaanza.

"Ni vitu vichache vya pamoja ndio vinasubiriwa, wote tuna hamu ya kumaliza msimu huu, tunataka kuwapa furaha mashabiki wetu, tunajua kiu yao," alisema Rweyemamu.

Simba ndio vinara na mabingwa watetezi wa ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari Kubwa