Simba: Yanga 'jeuri' itawaponza

27Jun 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Yanga 'jeuri' itawaponza

KLABU ya soka ya Simba imesema kuwa haijapokea barua yoyote kutoka kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Yanga inayomuombea ruhusa beki wake wa zamani, Hassan Kessy ili aweze kuitumikia timu yake mpya katika mechi dhidi ya TP Mazembe kutoka Kongo itakayofanyika kesho.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema kuwa klabu yake haina 'kinyongo' na uamuzi uliofanywa na mchezaji huyo, lakini hawawezi kutoa ruhusa bila ya kupokea maombi rasmi kama ilivyofanywa na Yanga mwaka 1998.

"Hakuna barua yoyote ambayo Yanga imetuandikia kuhusiana na suala la mchezaji Hassan Ramadhani 'Kessy', pia hakuna hata mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi wa vilabu hivi ili kutuomba walau kwa mdomo kama taratibu zinavyotaka," alisema Manara.

Mwaka 1998 Simba iliwaazima Yanga wachezaji wake watatu ili iwatumie katika mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ambao ni Shaaban Ramadhani, Monja Liseki na Alphonse Modest.

Aliongeza kuwa Simba ni waungwana na kukaa kwao kimya Yanga wasitumie nafasi hiyo kuwapotosha wanachama na washabiki wake kuwa wamekataliwa kumtumia Kessy katika michuano hiyo ya kimaraifa baada ya kumsajili.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa