Simba, Yanga kumaliza tambo

11Jul 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga kumaliza tambo
  • Mnyama ajipanga kuthibitisha ubora wake, huku Yanga wakiiota tiketi ya kushiriki michuano ya CAF...

ZAIDI ya kisasi! ndivyo kila upande kati ya Simba na Yanga unavyosema kuelekea mechi yao ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA inayotarajiwa kuchezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Mwamuzi wa kati wa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11:00 jioni, atakuwa ni Aboubakari Mturo, ambaye atasaidiwa na Abdallah Mwinyimkuu, Nadeem Aloyce, Ramadhani Kayoko, Frank Komba na Kassim Mpanga huku Kamisaa akiwa ni Ally Katolila.

Mechi hiyo itakuwa ni ya tatu kuwakutanisha msimu huu baada ya mchezo kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na waliporudiana Machi 8, mwaka huu, Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0.

Hata hivyo, mbali na kusaka heshima, mechi ya kesho ni mchezo wa mashindano yanayochezwa kwa mfumo wa mtoano na bingwa wake hupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Simba ilifika hatua hiyo baada ya kuwaondoa waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC kwa kuwafunga mabao 2-0, wakati Yanga ilisonga mbele kutokana na kuichapa Kagera Sugar magoli 2-1, mechi zote za hatua ya robo fainali zikichezwa jijini.

Licha ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa haijamalizika, mabingwa wa msimu huu, Simba watashuka dimbani tayari wakiwa na tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo yanasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenvroeck, alisema amejiandaa kukamilisha msimu wa 2019/20 vizuri na anaamini kikosi chake hakitarudia makosa yaliyofanywa kwenye mchezo uliopita.

Sven alisema anajua mechi hiyo ni ngumu na ndio tegemeo pekee kwa wapinzani wao Yanga kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Alisema wanahitaji kuongeza umakini na kucheza katika kiwango chao bora ili wapate matokeo chanya na hatimaye kuwaondolea machungu mashabiki wao wanaoumizwa na kipigo walichapata Machi 8, mwaka huu kutoka kwa watani zao.

"Tunahitaji kuwa makini na watulivu zaidi, mechi ya Jumapili ni mechi itakayokuwa na ushindani, changamoto mbalimbali pamoja na presha, tunatakiwa kutokuwa na papara, tunachotakiwa kufanya ni kutumia vema nafasi tutakazozitengeneza," Sven alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema wamejipanga kupata ushindi ili kuendelea na kampeni yao ya kuchukua vikombe msimu huu.

Manara alisema siri ya mafanikio ya timu yao msimu huu, imetokana na kuwa na kikosi imara ambacho kwa asilimia kubwa kitaendelea kuitumikia klabu hiyo tena katika msimu ujao.

"Tumejipanga, watatueleza walipataje ushindi Machi 8, au kama watabahatisha kwa mara nyingine, hawawezi," Manara alitamba.

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, aliliambia gazeti hili mechi ya kesho kwake ni muhimu zaidi kuliko mechi nyingine walizocheza msimu huu.

Eymael alisema si kama wanahitaji kuendelea kuifunga Simba, lakini wanahitaji kusonga mbele katika mashindano hayo ili watimize malengo ya kukichukua kikombe hicho na kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

"Ni mechi muhimu sana kwa Yanga, ni mechi ambayo itatupa mwelekeo wa kushiriki mashindano ya kimataifa, tunahitaji kushiriki mashindano ya CAF msimu ujao, hii ndio nafasi pekee tuliyonayo ili kufikia malengo, hatutaki kumaliza msimu huu bila kikombe, baada ya kupoteza taji la Ligi Kuu," Eymael alisema.

Mbelgiji huyo amewataka mashabiki wa Yanga kutokuwa na hofu na kuendelea kuungana ili wapate ushindi.

Mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga kati ya wenyeji Sahare All Stars dhidi ya Namungo FC kutoka Lindi.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Habari Kubwa