Simba, Yanga sasa vita Mapinduzi Cup

07Jan 2020
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Simba, Yanga sasa vita Mapinduzi Cup
  • *** Zapania kuipoka Kombe Azam FC, zapeleka vikosi kamili zikishuka dimbani leo Pemba na Unguja, huku....

BAADA ya kutoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, miamba ya soka nchini, Simba na Yanga zimehamishia vita mpya kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Meneja wa Yanga, Abeid Mziba, picha mtandao

Katika michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi visiwani hapa jana, licha ya timu hizo kupangwa makundi tofauti, kila moja imejigamba kulibeba taji hilo linalowaniwa na timu nane mwaka huu.

Yanga ambayo ipo Kundi A sambamba na Azam FC, Mlandege na Jamhuri itashuka dimbani leo usiku kuvaana na Jamhuri kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Na kwa upande wa Simba ambayo ipo Kundi B sambamba na Mtibwa Sugar na Chipukizi itavaana na Zimamoto katika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Hata hivyo, miamba hiyo ya Tanzania Bara msimu huu imeeleza kupania kutwaa ubingwa huo, ambao unashikiliwa na mabingwa watetezi, Azam FC ambayo jana usiku ilivaana na Mlandege katika Uwanja wa Amaan.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana kutoka visiwani hapa, mameneja wa timu hizo kongwe nchini, walijinasibu kutofanya makosa mwaka huu katika kinyang'anyiro hicho.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, akizungumza na waandishi wa habari alisema lengo lao ni kubeba Kombe la Mapinduzi na kwa kuonyesha dhamira hiyo wamekuja visiwani hapa na kikosi kamili.

"Leo (juzi) tumetangulia na wachezaji 17 wote hawa ni wa timu ya wakubwa isipokuwa mmoja tu ndiye anatoka timu B, wachezaji wangine watakuja baadaye.

"Wachezaji waliobaki Dar es Salaam ni wale tu walionza katika kikosi cha kwanza dhidi ya Yanga Jumamosi, ambao nao watawasili na kocha anaweza kuwatumia katika mechi ijayo (kama itasonga mbele)," alisema Rweyemamu.

Kwa upande wake Meneja wa Yanga, Abeid Mziba, alisema mwaka jana walileta Kikosi B, lakini mwaka huu wamekuja visiwani hapa wakiwa na kikosi kamili cha wakubwa.

"Lengo letu ni kutwaa ubingwa na tofauti na mwaka jana, mwaka huu tumekuja na kikosi kamili kuna wachezaji wachache tu tunatarajia wataungana na wenzao leo (jana) akiwamo Yondani (Kelvin).

"Mashabiki wetu wajitokeza kwa wingi kuja kuishangilia timu na tunaamini kwa mechi ya kesho (leo) dhidi ya Jamhuri, uzoefu na ukongwe utatubeba," alisema nyota huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

Michuano hiyo iliyoanza jana kwa Mtibwa Sugar kuvaana na Chipukizi katika Uwanja wa Gombani huku Dimba la Amaan Azam FC ikipepetana na Mlandege, mwaka huu inachezwa kwa mfumo wa mtoano.

Fainali ya michuano hiyo itapigwa katika Uwanja wa Amaan Januari 13, mwaka huu kwa kumkutanisha mshindi wa Kundi A na wa Kundi B kutoka Pemba.

Habari Kubwa