Simba, Yanga zaanza kusaka ufalme Ligi Kuu

06Sep 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba, Yanga zaanza kusaka ufalme Ligi Kuu
  • ***Kipyenga chapulizwa leo, viwanja vyarindima, timu zajivunia vikosi huku...

KIPENGA cha Ligi Kuu Bara kimepulizwa rasmi na leo mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba watashuka dimbani kuvaana na Ihefu FC katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, huku Yanga ikicheza na Prisons uwanja wa Benjamini Mkapa.

Simba itashuka dimbani ikiwa na morali ya hali ya juu, ikitaka kuendeleza mbio zake za ushindi baada ya kutoka kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Namungo FC mabao 2-0 kwenye mechi hiyo ya kufungua msimu iliyopigwa Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ushindi kwa Simba utatoa mwelekeo wa kuanza vema mbio za kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo katika mwezi huu wa Septemba ambao kwa mujibu wa ratiba ina mechi nne zitakazoiwezesha kuvuna pointi 12 endapo itashinda zote.

Baada ya mechi hiyo, Septemba 12, itashuka katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro kuivaa Mtibwa Sugar kabla ya Septemba 20, kuialika Biashara United katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Septemba 26, Simba itahitimisha ratiba yake ya mwezi huu kwa kuialika timu nyingine inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, Gwambina FC ya Misungwi jijini Mwanza, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumzia maandalizi ya ligi hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mechi hiyo ya ufunguzi leo, lakini akaweka wazi ligi ya msimu huu itakuwa ngumu zaidi.

Sven amesema timu zote zinaonekana kujiandaa vizuri ikiwa ni pamoja na kufanya usajili wa kuvutia, hivyo kila mechi itakuwa ngumu, lakini anaimani upana wa kikosi chake utamsaidia kupata matokeo.

"Timu zimesajili vizuri, lakini hata sisi tuna wachezaji wazuri katika kila nafasi, hivyo nitakuwa na uwanja mpana wa kupanga kikosi," alisema.

Kuhusu mechi ya leo, Sven alisema Ihefu ni timu ngeni katika ligi hiyo, lakini si ya kubeza, ila morali ya wachezaji wake na utayari wa mchezo unampa matumaini ya kuanza vizuri ligi hiyo.

Simba ambayo msimu uliomalizika wa 2019/20, imetwaa mataji matatu, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA Cup) na Ubingwa wa Ligi Kuu Bara, imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota wapya saba kuelekea msimu mpya wa 2020/21.

Katika safu ya ulinzi imeimarisha kwa kusajili mabeki wa kati wawili, Ibrahim Ame kutoka Coastal Union, Mkenya Joash Onyango mchezaji huru aliyemaliza mkataba wake Gor Mahia ya Kenya na beki wa kulia David Kameta 'Duchu' akitokea Lipuli FC.

Safu ya kiungo wa kati imemsajili Mzambia Rally Bwalya kutoka Lusaka Dynamos ya Zambia, huku winga ikimnasa Mghana Bernard Morrison aliyemaliza mkataba na Yanga.

Kwa upande wa safu ya ushambuliaji iliyokuwa chini ya Mnyarwanda Meddie Kagere na mzawa John Bocco, imeongezewa straika Mkongomani Chris Mugalu aliyejiunga na mabingwa hao akitokea Lusaka Dynamos pamoja na mzawa Charles Ilamya kutoka KMC FC.

Nyota hao ndio wanaomfanya Sven kujivunia kikosi kipana katika kila nafasi kutokana na uwezo binafsi wa kila mchezaji.

Kwa upande wake Yanga itaivaa Prisons kutoka Mbeya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakiwa na matumaini makubwa na kikosi chao msimu huu.

Yanga itaingia uwanjani ikiwa na wachezaji wengi wapya, ambao watakuwa na kazi ya kuwaonyesha mashabiki wa klabu hiyo kuwa kikosi cha msimu huu ni moto wa kuotea mbali, kutokana na gharama kubwa zilizotumika kuwasajili.

Wanachama na mashabiki watakaokuwa uwanjani na kwenye televisheni zao, leo watataka kuangalia kiwango kama kile kilichoonekana kwenye tamasha la Wiki ya Mwananchi kwenye uwanja huo Jumapili iliyopita ilipocheza dhidi ya Aigle Noir ya Burundi na kushinda mabao 2-0.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika kwenye kambi yao iliyopo Kimbiji maeneo ya Kigamboni na kikosi kina majeruhi mmoja tu ambaye ni Mapinduzi Balama.

"Balama bado majeruhi na inawezekana akakosekana kwa muda wa wiki mbili, lakini wote 26 wako sawasawa, na Kocha Mkuu Zlatko Krmpotic ameniambia vijana wako tayari kwa ajili ya mchezo," alisema Bumbuli.

Kwa upande wa Prisons imesema kuwa Yanga wasitarajie mteremko kwenye mechi hiyo ili kuwafurahisha mashabiki wao.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ajabu Kifukwe, alisema kuwa kikosi chao kipo Dar es Salaam kwa muda mrefu kuisubiri Yanga.

"Tuko Dar es Sakaan wiki mbili sasa, tunawaambia mashabiki wetu kuwa wasubirie furaha tu kwenye mechi hii ya kwanza, niwape tahadhari tu wapinzani wetu, wasitarajie mteremko kwani kikosi chetu msimu huu ni kizuri kuliko hata kile cha msimu uliopita," alisema Kifukwe.

Macho ya mashabiki wengi wa soka watakuwa kwa wachezaji wapya wa Yanga, hasa kina Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe, Michael Sarpong, Carlos Stenio Fernanders Guimaraes do Carmo Carlinhos na wengineo.

Mechi nyingine za Ligi hiyo ni Namungo vs Coastal Union, Biashara vs Gwambina, Mtibwa vs Ruvu Shooting na Dodoma vs Mwadui.

Lig hiyo itaendelea kesho wakati KMC itacheza na Mbeya City, huku Kagera ikiikaribisha JKT Tanzania na Azam kuivaa Polisi Tanzania.

Habari Kubwa