Simba, Yanga zatangaza vita

16Apr 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga zatangaza vita
  • ***Coastal, Mtibwa Sugar kazi wanayo kesho Mkwakwani na Jamhuri, makocha wasema...

WAKATI kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kikiwasili salama jijini Tanga jana mchana tayari kuwavaa wenyeji wao Coastal Union katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa CCM, Mkwakwani, watani zao Yanga wamesema hawakamatiki na wamejipanga ...

kuidunda Mtibwa Sugar siku hiyo.

Hata hivyo, Simba ambayo Jumamosi iliyopita walitolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imetua Tanga bila nyota wake watatu wa kimataifa ambao ni majeruhi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliwataja wachezaji hao ambao ni majeruhi ni pamoja na kiungo James Kotei, mabeki, Juuko Murshid na Paschal Wawa.

Rweyemamu alisema kuwa Kotei na Juuko waliumia katika mechi ya marudiano dhidi ya TP Mazembe wakati Wawa yeye aliumia katika mechi ya kwanza iliyochezwa hapa nchini na kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

"Tumeshafika Tanga, mechi ni Jumatano, lakini tumeamua kuja mapema kwa sababu ya kufanya mazoezi kwa utulivu, tunajua huu mchezo utakuwa mgumu kama mechi nyingine ambazo tumeshacheza za ligi, Simba ina malengo yake na wenzetu pia wana malengo yao," alisema Rweyemamu.

Meneja huyo aliongeza kuwa benchi la ufundi la timu hiyo lililoko chini ya Mbelgiji Patrick Aussems linajipanga kuandaa kikosi kitakachoshuka dimbani kwenda kulingana na wachezaji watakaokuwa tayari kwa mechi hiyo.

Taarifa kutoka Tanga zinaeleza kuwa kikosi cha Coastal Union kimekwenda Pangani kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo.

Pia taarifa zaidi zimeeleza kuwa timu hiyo huenda ikapata motisha kutoka kwa wafadhili wao endapo itafanikiwa kuondoka na ushindi kwenye mechi hiyo.

Baada ya mechi hiyo ya kesho, Simba yenye pointi 57 ikiwa imecheza mechi 22, itasafiri kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kucheza mechi nne dhidi ya Kagera Sugar, Alliance FC, KMC na Biashara United, ambazo zitachezwa ndani ya siku nane.

Kwa upande wa Yanga, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, amesema wamejipanga kuhakikisha wanashinda mechi yao ya kesho dhidi ya Mtibwa Sugar na hakuna timu ambayo itawasimamisha kwenye mbio zao za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mchezo huo wa raundi ya 32 kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga utachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuanzia saa 10:00 jioni.

Zahera alisema wachezaji wake wanajua malengo waliyokuwa nayo na wanaamini kutwaa ubingwa ndiyo kutawaweka katika nafasi nzuri ya maandalizi ya msimu mpya.

"Sijaona timu ambayo inaweza kutusumbua kama wachezaji wangu watafanya kile ninachowaelekeza, hakuna mechi ngumu, ila kuna ushindani kwenye ligi, tumefaulu kwa kushinda mechi zilizopita, na zilizoko mbele yetu pia tutahakikisha tunashinda, hayo ndiyo malengo yetu," alisema kocha huyo.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na jana jioni walitarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri akiwamo nahodha wao, Ibrahim Ajibu.

"Tutamkosa Yondani (Kelvin) kutokana na kadi nyekundu aliyopewa, Ninja (Shaibu) alishamaliza adhabu yake, Ajibu naye yuko fiti, mashabiki wetu watarajie kuona kiwango bora," alisema meneja huyo.

Yanga wenye pointi 74 ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati African Lyon ambao wamecheza mechi 33, wanaburuza mkia wakiwa na pointi 22.

Habari Kubwa