Simba, Yanga zazifuta Azam FC, Mtibwa Z'bar

09Jan 2020
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Simba, Yanga zazifuta Azam FC, Mtibwa Z'bar
  • ***Mashabiki waziombea zitinge fainali washuhudie 'dabi', Bocco na Banka watoa neno...

BAADA ya Yanga juzi usiku kuungana na Simba, Azam FC na Mtibwa Sugar kutinga nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi habari ya mjini visiwani hapa sasa ni 'dua' kwa timu hizo kongwe nchi kukutana fainali.

Yanga imetinga nusu fainali baada ya kuichapa Jamhuri kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimyani na Adeyum Saleh na Mohamed Issa 'Banka' dakika ya 45 na 85 kwenye Uwanja wa Amaan juzi usiku.

Wakati Simba yenyewe ikitinga nusu fainali juzi jioni kwa kuichapa Zimamoto 3-1 shukrani kwa mabao ya John Bocco, Sharaf Shiboub na Ibrahim Ajibu.

Kwa upande wa Azam na Mtibwa zilizitoa Mlandege na Chipukizi kwa ushindi wa 1-0 na mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare bao 1-1.

Hata hivyo, wakati Yanga ikishuka dimbani leo saa 2:15 usiku kuvaana na Mtibwa Sugar katika nusu fainali ya kwanza kabla ya Simba kesho majira kama hayo kuvaana na mabingwa watetezi, Azam FC mashabiki visiwani hapa maombi yao ni kuona watani hao wa jadi wakikutana fainali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya Yanga kutinga nusu fainali, waliliambia Nipashe kuwa wanatamani kuona Mtibwa na Azam zikitolewa ili washuhidie 'dabi' ya watani hao.

Kocha wa Jamhuri, Mustafa Hassan 'Mu', baada ya timu yake kuangukia kipigo, alisema anaziona Simba na Yanga zikitinga fainali ingawa mpira ni dakika 90 na lolote linaweza kutokea.

"Wapenzi wengi wasoka wanataka Simba na Yanga zikutane fainali, jambo ambalo hata mimi natamani hivyo, lakini ukumbuke Azam ni wazoefu wa michuano hii na wapo vizuri wakitaka kutetea ubingwa wao.

"Ila tofauti na miaka mingine mwaka huu naona Simba na Yanga zimedhamiria ubingwa na zimeleta vikosi kamili, nadhani zinaweza kukutana," alisema.

Nassor Juma, mdau wa soka ambaye hakuwa tayari kueleza yeye ni shabiki wa timu ipi kati ya Simba na Yanga, alisema: "Ni wakati wa Wazanzibar kushuhudia dabi kwenye Uwanja wa Amaan, hivyo dua zangu Azam na Mtibwa zitolewe."

Straika wa Yanga aliyerejea katika makali yake akitokea chumba cha majeruhi, Banka alisema hesabu zao kwanza ni kwa Mtibwa na hawaihofii timu yoyote.

"Simba tumekutana nayo wiki iliyopita, hatuna hofu tumekuja kupambana na lengo letu ni kutwaa kombe tupo tayari kucheza na timu yoyote," alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Kocha msaidizi wa Yanga, Said Maulid aliyepo visiwani hapa na timu, ambapo alisema mechi zote ni ngumu lakini walichofuata ni kombe hivyo wapo tayari kukutana na Simba kama ikitokea.

Kwa upande wake nahodha wa Simba, John Bocco, alisema wamekuja kupambana na wanatambua Azam ni timu kubwa lakini wanachotaka ni kombe tu.

Alisema baada ya kulikosa kombe hilo mwaka jana kwa kupoteza mechi ya fainali dhidi ya Azam, safari hii hawataki kurudia makosa hayo tena.

Habari Kubwa