Simba yaonywa straika mmoja

17Sep 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaonywa straika mmoja

KIPA wa zamani wa Simba, Steven Nemes, ameonya kuwa timu hiyo ikiendelea kutumia straika mmoja, itapata tabu sana kupata ushindi kwenye mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara, badala yake inatakiwa itumie mastraika wawili.

Nemes ambaye kabla ya kuhamia Simba alikuwa akiichezea Yanga, alisema kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck anafanya makosa kumchezesha straika mmoja mbele jambo ambalo anaifanya timu yake kupata tabu sana ya kushinda, kwa sababu tayari baadhi ya makocha wameshagundua mbinu yake.

"Kwanza kabisa kuchezesha straika mmoja ni lazima awe na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kukaa nao kwa sekunde kadhaa, mwenye nguvu ya kuweza kukabiliana na mabeki wawili au watatu wa timu pinzani, na pia asiwe anatoka sana kwenye eneo la goli kwenda kutafuta mpira sehemu nyingine," alisema Nemes.

Aliongeza kuwa Bocco, pamoja na kuwa na sifa ya kukaa na mpira na nguvu, lakini ana tabia ya kutoka kwenda nyuma, kati na pembeni, hivyo eneo la kati linakuwa halina mtu, hivyo safu hiyo ya ushambuliaji inapwaya.

"Kama Bocco akiwa na Kagere, basi mmoja anatoka kwenda pembeni au kati, lakini mmoja anabaki eneo la hatari na hii huwa inawasaidia sana Simba kupata ushindi tena wa mabao mengi, lakini hii ya straika mmoja inakuwa na matatizo kwa sababu, hata viungo ambao wamewekwa ili wamsaidie kumlisha straika mmoja, nao bado hawafanyi kazi yao vizuri, hilo ni tatizo," alisema.

Nemes pia alisema kwenye mechi za mikoani ambako viwanja si vizuri sana ndiyo tatizo linakuwa kubwa zaidi, hivyo angalau awe hivyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini viwanja vya mikoani straika mmoja ni tatizo zaidi kutokana na staili ya ucheza wa Simba, hivyo kumtaka kocha huyo abadilike kama anataka kutetea ubingwa wao.

Habari Kubwa