Simba yapapaswa, Azam ikifia Mtibwa

27Oct 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yapapaswa, Azam ikifia Mtibwa
  • ***Mechi yageuka ya kibabe Uhuru, huku Wanalambalamba nao wakilambishwa...

WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakipoteza mechi yao ya pili mfululizo baada ya jana kukubali kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mtibwa Sugar nayo imewatuliza vinara wa ligi hiyo, Azam FC kwa kichapo kama hicho.

Kipigo hicho kinaifanya Simba kuendelea kupata tabu dhidi ya timu za majeshi baada ya Alhamisi iliyopita, kupoteza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu ilipotandikwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.

Lakini, ushindi huo kwa Ruvu Shooting ni mwendelezo wa kufanya vizuri baada ya mchezo uliopita kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC, huku wababe waliopita wa Simba, Prisons nao jana wakiendeleza ushindi kwa kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0 kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Katika mechi ya Simba na Ruvu Shooting, alikuwa ni Fully Maganga aliyepeleka msiba Msimbazi, akifunga bao dakika ya 35 baada ya timu yake kufanya shambulizi la kushtukiza.

Baada ya Simba kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Ruvu Shooting, ulipigwa mpira mrefu ambao ulisababisha kizaazaa kwenye lango la Simba na kumkuta mfungaji aliyeachia shuti la karibu lililomshinda kipa Beno Kakolanya na kajaa wavuni.

Kuanzia dakika ya 70, mechi hiyo ilisimama kwa muda kutokana na wachezaji wa pande zote mbili kusukumana kwa hasira, hali hiyo ikitokana na mchezaji wa Ruvu kumchezea rafu Luis Miquissone ambayo ilizaa penalti.

Hata hivyo, nahodha wa timu ya Simba, John Bocco, ambaye ni aghalabu sana kukosa penalti, aligongesha mlingoti wa juu na kurejea uwanjani dakika ya 78, akiikosesha timu yake bao la kusawazisha.

Mechi ilianza kwa kasi na dakika ya sita, Ibrahim Ajibu aliunganisha kwa kichwa mpira wa krosi kutoka kwa Larry Bwalya, lakini ulitoka kidogo nje la lango la Ruvu Shooting.

Dakika ya 20, Abdulrahman Mussa alibaki yeye na kipa Kakolanya, lakini alipiga nje. Lilikuwa ni shambulizi la kushtukiza baada ya Simba kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Ruvu Shooting.

Luis Miquissone, alikosa bao la wazi dakika ya 34 alipobaki yeye na kipa wa Ruvu, lakini akamlenga na kipa akaudaka kirahisi mpira huo. Dakika moja kabla ya mapumziko, Shomari Kapombe aliikosesha Simba bao la kusawazisha akiwa amebaki na lango akapiga mpira juu.

Kipindi cha pili, Simba iliwatoa Bwalya na Francis Kahata na nafasi zao kuchukuliwa na Bocco, pamoja na Bernard Morrison, licha ya kujitahidi kuleta uhai, lakini mabeki wa Ruvu Shooting wakiongozwa na Juma Nyosso walikaa imara kuokoa hatari zote, huku wakitumia nguvu zaidi kuwazuia wachezaji wa Simba.

Kwingineko katika Uwanja wa Jamhuri,  Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar waliwaonjesha vinara wa Ligi Kuu, Azam FC kipigo cha kwanza msimu huu kwa kichapo cha bao 1-0, shukrani kwa Jafar Kibaya aliyewazamisha dakika ya 61 kwa shuti kali la mbali ambalo lilimshinda kipa David Kisu.

Kwa matokeo hayo ya jana Simba inabaki na pointi zake 13, ikiwa nafasi ya nne wakati Azam nayo ikiendelea kubaki kileleni na alama zake 21, Tanzania Prisons inapanda hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi 12, huku Ruvu Shooting yenye pointi 12 ikiwa nafasi ya saba na Mtibwa nafasi ya 10 ikiwa na alama 11.

Habari Kubwa