Simba yashindwa kuishusha Azam

12May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba yashindwa kuishusha Azam

SIMBA ya Dar es Salaam imeendelea kusuasua baada ya kutoka suluhu na timu ya Majimaji katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini hapa.

majimaji vs simba

Sare hiyo ya jana ni ya tano kwa Simba msimu huu na inaifanya ifikishe pointi 59 na kushindwa kuishusha Azam FC yenye pointi 60 iliyokuwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Mei 21.

Majimaji ambayo katika mechi ya mzunguko wa kwanza ilipata kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa Simba jana ilifikisha pointi 34.

Kikosi cha Kocha Mkuu wa Simba Jackson Mayanja ambaye jana alirejea kwenye benchi baada ya kumaliza adhabu yake ya kukosa mechi mbili zilizopita dhidi ya Azam na Mwadui FC jana kilionekana kucheza soka la 'kupooza' na kikianza bila ya nyota wa kigeni.

Dakika ya 35 Simba walikaribia kupata bao kupitia kwa kiungo wake Said Ndemla lakini shuti alilopiga lilidakwa na kipa wa Majimaji na kuwanyima Msimbazi nafasi ya kufunga.

Kipindi cha pili kilipoanza Simba walionekana kucheza pasi nyingi zaidi katikati ya uwanja na kushindwa kutengeneza nafasi za kufunga tofauti na ilivyokuwa kwenye dakika 45 za awali.

Simba inatarajiwa kuondoka leo mkoani hapa na kwenda kuweka kambi Morogoro kwa ajili ya kuwasubiri Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi hiyo utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Simba; Peter Manyika, Said Issa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mohammed Fakhi, Hassan Isihaka, Novaty Lufunga, Said Ndemla, Abdi Banda, Mussa Hassan 'Mgosi' na Peter Mwalyanzi/ Justice Majabvi (dk 57).

Habari Kubwa