Simba yatamba imepata 'dawa'

22Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yatamba imepata 'dawa'
  • ***Ni katika kuelekea mchezo wa watani huku Yanga ikiwaambia...

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba Mfaransa Didier Gomes amesema ameshapata 'dawa' ya kuondoka na ushindi katika mechi ya fainali ya Kombe la FA, uongozi wa Yanga wenyewe umeweka wazi kikosi chao kiko imara kuhakikisha wanaendeleza ubabe dhidi ya watani zao.

Simba na Yanga zinatarajia kukutana katika mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la FA itakayochezwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Akizungumza na gazeti hili jana, Gomes alisema kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi amepata muda wa 'kuisoma' na kuipeleleza Yanga na kuweka mipango ya kuwamaliza.

Gomes alisema kikosi chake kimeshabaini mahali walipokosea, hivyo kamwe hawatarudia kosa hilo kwa ajili ya kuhakikisha wanatetea ubingwa wa michuano hiyo ambao wanaushikilia.

"Tumepata muda wa kukaa na kupitia mkanda wa video ya mchezo uliopita dhidi ya Yanga na kubaini upungufu na ubora wa wapinzania wetu, lakini tumeangalia na mechi zao nyingine kwa ajili ya kujifunza na kujiimarisha kwa kuangalia makosa yao," alisema Gomes.

Aliongeza wamejipanga kuhakikisha wanafuta machungu ya kupoteza mchezo wao wa mwisho ambao walilala kwa bao 1-0.

"Katika mazingira yoyote, ninaahidi kuondoka na ushindi, tunakwenda kwenye fainali kulipa kisasi kwa Yanga," Gomes alisema.

Aliongeza lengo lao ni kuona wanamaliza msimu huu kwa heshima na kushinda mchezo huo ndio jambo pekee wanalosubiri kuona linatimia.

Alisema tayari ameshapata 'dawa ya kumaliza' Yanga ambao ni kutumia washambuliaji watatu kama alivyofanya katika dakika za mwisho za mchezo dhidi ya Namungo FC ambapo aliwatumia kwa pamoja washambuliaji wake watatu ambao ni Chris Mugalu, Meddie Kagere na nahodha John Bocco.

"Unajua kuwatumia Bocco, Mugalu na Kagere kwa pamoja maana yake ni mwendo wa kushambulia na kutaka kupata bao, kama ilivyo katika michezo miwili ya mwisho, tutakwenda na mfumo huo kwa sababu tunahitaji kutetea taji la FA," alisema Gomes.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, aliliambia gazeti hili wanaimani na kikosi chao na wamejiandaa kwenda kufunga msimu wa 2020/21 kwa kishindo.

"Viongozi tuna imani na wachezaji na benchi la ufundi katika kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu, tutaendelea kusajili wachezaji bora ili tufanye vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tutajiimarisha ili kufanikisha hilo na hapa nyumbani hizi ‘back to back’ zitakuwa nyingi sana,” alisema Barbara.

Naye Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema timu yao iko imara na wanakwenda Kigoma kwa kazi moja ya kuchukua kikombe cha mashindano hayo.

Nugaz alisema wao wanahitaji ushindi ili kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa nguvu zao.

"Sisi tunajua kujiandaa kwa ajili ya kuifunga Simba, mechi ya FA imeshamalizika," Nugaz alisema kwa kifupi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara ameamua kuachana na klabu hiyo kwa kile alichosema amechoka 'kuandamwa'.

"Hivi vitimbi mnavyonifanyia kila siku kisa Simba vishanichosha, mwisho wa siku mtanitoa roho yangu kabla ya muda wangu. Imetosha kwa sasa," alisema Manara.

Katika hatua nyingine, mwamuzi kutoka Manyara, Ahmed Arajiga ameteuliwa kuchezesha mchezo huo wa watani wa jadi akishirikiana na Fredinand Chacha (Mwanza), Mohamed Mkono (Tanga) na Elly Sasii wa Dar es Salaam.

Habari Kubwa