Simba yateseka  Lipuli ikiivuta mkia

22Apr 2018
Somoe Ng'itu
IRINGA
Nipashe Jumapili
Simba yateseka  Lipuli ikiivuta mkia

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba, wamepunguzwa kasi katika mbio zake za kuwania ubingwa baada ya kuteseka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Lipuli FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Samora mjini hapa.

Mshambuliaji wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’, akicheza mpira kwa kichwa katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa jana na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1. PICHA: SOMOE NG'ITU

Kutokana na matokeo hayo, Simba sasa imefikisha pointi 59 wakati Lipuli wao wakifikisha pointi 32 wakiwa wamejiondoa kwenye janga la kushuka daraja.

Mchezaji Bora wa mwezi uliopita, Adam Salamba, ndiye aliyewafungia Lipuli bao hilo katika dakika ya 31 baada ya kumzungusha beki wa Simba, Yusufu Mlipili, na kupiga shuti lililomshinda kipa wa vinara hao, Aishi Manula.

Laudit Mavugo aliyeingia kuchukua nafasi ya Juuko Murshid alifunga bao la kusawazisha baada ya kuwahi mpira wa kona uliopigwa na Shomary Kapombe kufuatia mabeki wa Lipuli kuchelewa kuokoa hatari hiyo katika lango lao katika dakika ya 65.

Bao hilo la Salamba lilidumu mpaka timu hizo zilipokwenda mapumziko.

Hata hivyo Lipuli walionekana kuwa vizuri zaidi katika kipindi cha kwanza kwa kucheza kwa kujiamini na kufuata maelekezo ya kocha wao, Selemani Matola, anayesaidiana na Amri Saidi.

Emmanuel Okwi alikaribia kuipatia Simba bao la mapema, lakini frikiki aliyopiga katika dakika ya tatu ilitoka nje huku dakika mbili baadaye Lipuli wakijibu shambulizi hilo kupitia kwa Darytesh Saliboko, lakini shuti alilopiga akiwa na Manula lilitoka nje.

Dakika ya nane, Salamba, alimpiga chenga beki wa Simba, Juuko Murshid, lakini shuti alilopiga lilidakwa na Manula na kupoteza nafasi hiyo ya kuifungia Lipuli wakati John Bocco wa Simba naye alipiga pembeni mpira na kushindwa kufunga katika dakika ya 22.

Kipa Manula alidaka kiufundi shuti lililopigwa na straika wa Lipuli, Malimi Busungu, ambaye aliwahi kuichezea Yanga baada ya kupata pasi kutoka kwa Seif Abdallah na kuwanyima wenyeji hao nafasi ya kufunga katika dakika ya 35 wakati Mohamed Ali alipangua shuti la Shiza Kichuya dakika ya 38.

Dakika ya 79 Okwi alipiga krosi nzuri, lakini Mavugo aliyekuwa jirani na nyavu akapiga juu na kupoteza nafasi ya kuifungia timu yake bao lingine katika mchezo huo uliochezeshwa na refa, Hans Mabena.

Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo kwa Mbeya City kuwakaribisha mabingwa watetezi Yanga kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya.

 

Habari Kubwa