Simba yatetemesha Afrika

14Feb 2021
WAANDISHI WETU
Dodoma
Nipashe Jumapili
Simba yatetemesha Afrika
  • ***Ni baada ya kuweka rekodi ya kupata ushindi ugenini, pongezi zamiminika...

USHINDI wa bao 1-0 ilioupata Simba ikiwa ugenini nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), dhidi ya AS Vita katika mechi ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika umeijengea heshima timu hiyo na kuwapa furaha wadau mbalimbali wa soka hapa nchini.

Kwa muda mrefu AS Vita imekuwa ikizionea timu za Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuzipa vichapo kila inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, lakini juzi kibao kiliwageukia Wakongomani hao.

Straika mzaliwa wa nchi hiyo, Chriss Mugalu, aliipatia Simba bao pekee katika mchezo huo kwa penalti dakika ya 61 kufuatia shuti la Luis Miquissone kumgonga mkononi, Qusmane Quttara na mwamuzi kuamuru tuta lipigwe.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema amefurahishwa na ushindi huo na kuongeza ni mwanzo mzuri wa kuelekea kufanya vyema kwenye kundi hilo.

"Tunafuraha na tumeridhika na ushindi tulioupata kwa sababu tumecheza vizuri na tumepata matokeo mazuri kwa timu yetu ambayo yatatusaidia baadaye kwenye hatua hii ya makundi," alisema Gomes.

Kocha huyo alisema amefurahishwa na jinsi wachezaji wake walivyopambana na kucheza kwa kufuata maelekezo aliyowapa kwa sababu kila mmoja alifahamu AS Vita si timu ya mchezo.

"Unajua michuano hii ni lazima ucheze kwa mbinu zaidi. Niliwaambia vijana wangu kutowapa nafasi wapinzani ya kusogea hatua nyingi zaidi wakiwa na mpira. Nikawaelekeza jinsi ya kucheza wakiwa na mpira na wakiwa hawana, AS Vita ni timu inayojua kufanya mashambulizi ya kushtukiza, hasa mnapojisahau na kupanda mbele," alisema Didier.

Nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' , alisema wametimiza kile ambacho walitumwa na Watanzania kwenda kukifanya na wametimiza, huku akishukuru mapokezi mazuri waliyoyapata nchini humo.

"Ni mara ya pili nawaona mkicheza hapa. Mwaka 2018 tulitoka tumenyong'onyea, lakini mechi hii mmecheza kwa kujiamini. Tangu mwanzo niliongea na nyinyi machoni niliona ushindi, na haikuwa na kubahatisha, mmeonyesha uwezo mkubwa sana na mmeipa heshima kubwa nchi yetu," Balozi wa Tanzania DRC, Luteni Jenerali Mstaafu, Paul Mella alisema.

Balozi huyo alisema mtu wa kwanza kumpigia simu baada ya mechi kumalizika alikuwa ni Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa ushindi huo wa kihistoria.

 

SHANGWE BUNGENI

KAMA ilivyo ada, ushindi huo wa Wekundu wa Msimbazi umelitikisa bunge huku serikali ikitoa pongezi na kusema ni ushindi wa uchumi wa kati.

Hali hiyo ilijitokeza jana kwenye hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba.

Akitoa hotuba ya kuahirisha bunge jana, Waziri Mkuu alipongeza timu hiyo pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez kwa ubunifu wa kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii na hivyo kulipa heshima taifa kwa kulitangaza kupitia jezi yao yenye maneno ‘Visit Tanzania’.

“Kwa mujibu wa maelezo yake, neno ‘Visit Tanzania’ linakadiriwa kutazamwa na wapenzi wa soka takriban milioni 500 kutoka sehemu mbalimbali duniani, kupitia vituo vya Televisheni vya Canal Algérie, BeIN Sports, Eurosport, ESPN, Arryadia, GTV ya Ghana, MENA beIN Sports na West Africa Canal na imeshuhudiwa kwenye mchezo wa jana (juzi),”alisema.

Akijibu hoja za wabunge waliochangia Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano, Waziri Mwigulu alisema “Tanzania hatukufanya maombi wala kulipia kuingia uchumi wa kati bali ni jambo lililozingatia vigezo…Wewe unayepinga kwanini? Unaona sifa kuitwa maskini? Tunaona hata timu ya Simba kushinda juzi ni uchumi wa kati maana viwango vyao vilikuwa vya uchumi wa kati.”...

Habari Kubwa