Simba yatuma salamu Nigeria

23Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe Jumapili
Simba yatuma salamu Nigeria
  • Bocco apiga 'hat-trick' wakati Mnyama akiisulubu Coastal Union mabao 7-0, Azam hoi...

NAHODHA wa Simba, John Bocco, amefunga 'hat-trick' yake ya kwanza msimu huu huku mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakitoa kipigo kizito cha mabao 7-0 kwa Coastal Union katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha jana.

Mshambuliaji wa Simba, John Bocco (katikati), akijiandaa kuwatoka wachezaji wa Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha jana. Simba ilishinda mabao 7-0. PICHA: MTANDAO

Baada ya mechi ya jana, Simba itaendelea na maandalizi ya kuwafuata Plateau FC ya Nigeria kwa ajili ya mechi ya kwanza ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa mwishoni mwa wiki.

Kwa mabao hayo, Bocco anakwea hadi kileleni katika orodha ya wafungaji msimu huu baada ya kufikisha mabao saba, akiwaacha, Prince Dube wa Azam FC na Adam Adam wa JKT Tanzania ambao wana magoli sita kila mmoja.

Kwenye mechi hiyo, winga wa Simba, Bernard Morrison, alifunga bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini pia ni bao lake la pili kwa timu hiyo, akifanya hivyo kwenye uwanja huo huo, alifunga bao la pili kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 30, mwaka huu, Simba ikiichapa Namungo mabao 2-0.

Hii si mara ya kwanza, kwani misimu miwili iliyopita, 2018/19, Coastal ilipata kichapo cha mabao 8-0 kutoka kwa Simba kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, mechi iliyochezwa Machi 8, mwaka 2019.  

Dalili za Simba kupata mabao mengi, zilianza kuonekana mapema tu kwenye dakika ya nne, wakati mabeki wa Coastal Union walipomsahau kiungo, Hassan Dilunga wakidhani ameotea, lakini alikokota sana na kuchelewa kupiga, akakutwa na mabeki wa timu hiyo wakaokoa kabla hajafanya kitu chochote.

Dilunga alirekebisha makosa yake dakika mbili baadaye alipopachika bao la kwanza, kufuatia 'kumlamba' chenga kipa wa Coastal Union, Aboubakar Abbas na kuujaza wavuni, baada ya kupata pasi kutoka kwa nahodha wake, Bocco.

Faulo la dakika ya 14 iliyopigwa na Claotus Chama, nusura ilipatie Simba bao ilipogonga nguzo na kurejea uwanjani, huku kipa Abbas akiwa ameshakubali matokeo.

Kuanzia dakika ya 24, Bocco alianza kufanya shughuli yake, kwa kupachika bao la pili kwa Simba, akimalizia pasi safi kutoka kwa Diunga na wakati wachezaji wa Coastal wakishangaa, wasijue nini kimetokea, dakika mbili baadaye Bocco tena alifunga bao la tatu ambalo lilitokana na kupokea pasi kutoka kwa Morrison.

Nahodha huyo aliingia kwenye orodha ya kuwa mfungaji wa pili wa 'hat-trick' msimu huu baada ya Adam Adam wa JKT Tanzania, kwenye dakika ya 39, alipoupata mpira akiwa katikati ya mabeki wawili wa Coastal Union, akageuka na waacha huku wakimsukuma, lakini alipepesuka na alipokaa sawa, alitisha mara mbili kama anapiga, ya tatu akaachia shuti la juu lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni.

Adam alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga 'hat-trick', Oktoba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, alipofunga mabao matatu katika mchezo uliomalizika kwa JKT Tanzania kushinda mabao 6-1 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC.

Inaonekana kama Uwanja wa Sheikh Amri Abeid unampenda Morrison, kwani alirejea tena hapo na kufunga tena bao dakika ya 45 likiwa ni bao la tano, alipoupata mpira pembeni, kauweka kifuani kabla ya kuvuta hatua kadhaa na kuachia shuti la 'mwandamo wa mwezi' lililojaa pembeni mwa goli, ukimshinda kipa Abbas.

Kipindi cha pili kilipoanza, Kocha Sven Vandernbroeck, alimpumzisha Bocco na  nafasi yake kuchukuliwa na Ibrajim Ajibu ambaye alitoa pasi ya kisigino dakika ya 59 kuelekea kwa Chama, akiwa ndani ya eneo la hatari alipiga shuti hafifu kwa mguu wa kushoto na kuandika bao la sita.

Ni chama tena aliyepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Coastal Union, alipofunga bao la saba dakika tano kabla mechi kumalizika kwa mkwaju wa faulo, iliyotokana na Morrison kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari.

Kwa matokeo hayo, Simba inafikisha pointi 23, magoli 29 ya kufunga, ikifungwa matano, lakini ikiendelea kuwa kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Azam na Yanga, huku Coastal Union ikiwa kwenye nafasi ya 13 kwa pointi 12, timu zote zikiwa zimecheza mechi 11.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, KMC imeibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Azam FC na goli hilo pekee likifungwa dakika ya 59 na Reliant Lusajo aliyeunganisha pasi ya Kelvin Kijiri.

Timu zote zilifanya mashambulizi mbalimbali lakini Azam wataendelea kukumbuka shuti la dakika ya 25 la Prince Dube ambalo liligonga mwamba wa juu na dakika moja baadaye alikosa nafasi nyingine kwa mpira wa kichwa aliopiga kugonga mwamba wa chini.

Polisi Tanzania yenyewe ililazimishwa sare ya bila kufungana na Ihefu katika mechi iliyochezwa mapema jana mchana kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida

Habari Kubwa