Simba yavunja mwiko wa Mbeya City Taifa

09Mar 2016
Adam Fungamwango
Dar
Lete Raha
Simba yavunja mwiko wa Mbeya City Taifa

Mbeya City imeifungwa na Simba kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa tangu timu hiyo ilipopanda daraja na kucheza Ligi Kuu msimu wa 2013/14.

Mombeki na mabeki wa Mbeya City.

Haikuwa kazi rahisi Simba kuvunja mwiko huo. Ilibidi ipigane kwa saa moja na robo, ndipo ilipofanikiwa kupata bao lake la kwanza likiwekwa wavuni na straika Danny Lyanga dakika ya 75.

Bado haikuwa salama kwa Simba, kwani nusura Mbeya City isawazishe bao dakika za mwisho kama si juhudi za beki Juuko Mushid kuuokoa mpira, ni dhahiri ungetinga wavuni.

Wanachama na mashabiki wa Simba walipata uhakika wa kuondoka na pointi zote tatu pale Ibrahim Ajibu alipofunga bao maridadi, lililofanya timu hiyo kuifunga Mbeya City kwa mara kwa kwanza kwenye uwanja huo.

Kwa matokeo hayo Simba imeweka rekodi ya kuifunga timu hiyo mara zote mbili 'nje ndani' kwenye Ligi Kuu msimu huu, ikiwa pia ni mara ya kwanza kuifunga timu hiyo msimu huu tangu ipande, ikifanya hivyo nyumbani na ugenini.
Mwandishi wa makala haya, amekusanya matokeo ya mechi zote kati ya timu hizo na wafungaji.

1. Simba 2-2 Mbeya City (2013)

Ni mechi ya kwanza kati ya Simba na Mbeya City kuchezwa tangu timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya jiji la Mbeya kupanda daraja.

Ilikuwa ni Ligi Kuu msimu wa 2013/14, mechi ikichezwa Septemba 21, 2013 Uwanja wa Taifa na timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.

Amissi Tambwe ambaye kwa sasa yupo Yanga, aliifungia Simba magoli yote mawili, Paul Nonga ambaye kwa sasa naye yuko Yanga na Richard Peter wakifunga magoli kwa upande wa Mbeya City.

2. Mbeya City 1-1 Simba (2014)

Ilikuwa ni mechi ya marudiano mzunguko wa pili 2013/14 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya timu hizo zilipotoka tena sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 15, 2014 Tambwe aliifungia Simba bao. Awali Deogratius Julius aliifungia Mbeya City bao kwa mkwaju wa penalti.

3. Simba 1-2 Mbeya City (2014)

Simba ilipokea kichapo cha mabao 2-1 nyumbani Uwanja wa Taifa Januari 28, 2015 ikiwa ni Ligi Kuu msimu wa 2014/15.
Ibrahim Ajibu alikuwa ameifungia Simba bao, lakini baadaye Hamadi Kibopile aliisawazishia Mbeya City bao, kabla ya Yusuph Abdallah kushindilia bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 1 ya nyongeza, zilipoongezwa tano.

4. Mbeya City 2-0 Simba (2015)

Bado Simba haikuwa na dawa ya kuizuia Mbeya City, ilipokubali kipigo kingine kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa ligi 2014/15 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kilikuwa ni kipigo cha mabao 2-0, kilichopatikana Aprili 18, 2015.
Waliopeleka msiba Simba walikuwa ni Nonga na Peter Mwalyanzi ambaye kwa sasa amesajiliwa na timu hiyo ya Simba.

5. Mbeya City 0-1 Simba (2015)

Hatimaye msimu huu wa 2015/16 Simba ilifanikiwa kuvunja mwiko wa kutoifunga Mbeya City, ilipofanya hivyo ugenini Uwanja wa Sokoine kwa bao 1-0 lililofungwa mapema tu dakika ya pili na beki Juuko Murshid, mechi iliyopigwa Oktoba 17, 2015.

6. Simba 2-0 Mbeya City (2016)
Pamoja na kuivunja mwiko wa kutoifunga Mbeya City, rekodi bado zilionyesha kuwa haijawahi kuifunga kwenye Uwanja wa Taifa.
Jumapili iliyopita Simba ikafanya hivyo kwa mabao ya Danny Lyanga na Ibrahim Ajibu.

Habari Kubwa