Simba yawafuata AS Vita bila Bocco

17Jan 2019
Somoe Ng'itu
***Yakwea pipa na nyota 19 kuelekea DR Congo tayari kwa Jumamosi kuivaa...
Nipashe
Simba yawafuata AS Vita bila Bocco

MSHAMBULIAJI na nahodha wa Simba, John Bocco, si miongoni mwa wachezaji 19 wa timu hiyo wanaotarajiwa kusafiri leo asubuhi kuelekea mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwafuata wenyeji wao AS Vita, imefahamika.

MSHAMBULIAJI na nahodha wa Simba, John Bocco, picha mtandao

Bocco anaungana na mchezaji mwingine wa kikosi cha kwanza cha ‘Wekundu wa Msimbazi’ hao, beki tegemeo, Erasto Nyoni,
ambaye aliumia wakati wakishinda 1-0 katika mechi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM, kuukosa mchezo huo wa kwanza ugenini wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

AS Vita inatarajia kuwakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, katika mechi ya pili ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D itakayochezwa Jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kuwa Bocco bado ana maumivu ya misuli na anahitaji muda wa wiki moja ili kupona.

"Timu itaondoka kesho (leo) asubuhi ikiwa na wachezaji 19, ila mpaka sasa naweza kukwambia Bocco na Nyoni ndio hawako katika mipango ya safari," alisema kwa kifupi kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo inayowakilisha Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani humu.

Chanzo hicho kilisema pia tayari serikali imewahakikishia usalama wa msafara wa timu hiyo utakaoelekea Kinshasa na wanachotakiwa kufanya ni kuendelea na maandalizi mengine ya kusaka ushindi.

Waamuzi walioteuliwa kuchezesha mchezo huo ni Mahamadou Keita kutoka Mali atakayekuwa katikati na kusaidiwa na Seydou Tiama wa Burkina Faso na Sidiju Sidibe kutoka Guinea.

Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 3-0 walioupata katika mechi ya kwanza waliyocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya JS Saoura ya Algeria na kukaa kileleni katika kundi lao, wakati AS Vita yenyewe ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo cha mabao 2-0 ugenini dhidi ya Al Ahily ya Misri.

Habari Kubwa