Simba yawatesa Waarabu

13Jan 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba yawatesa Waarabu
  • ***Kocha JS Saoura asema alijiandaa kupokea kichapo huku akieleza timu yake...

BAADA ya timu yake kupata kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa JS Saoura, Nabil Neghiz amesema kuwa wapinzani wao ni wazuri na walicheza katika kiwango cha juu katika mchezo huo uliochezwa kwenye Dar es Salaam

Kwa matokeo hayo, Simba ambayo jana ilicheza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, imeondoka na pointi tatu muhimu, huku mechi nyingine ya Kundi D katika michuano hiyo kati ya Al Ahly ya Misri dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikitarajiwa kuchezwa jana usiku.

Akizungumza baada ya mechi hiyo jana, Neghiz alisema kuwa timu yake bado ni changa na tangu walipokuwa wanakuja Tanzania, alijua anakutana na timu yenye uzoefu na ngumu.

Kocha huyo aliongeza kuwa Simba ilicheza vizuri na ilistahili kupata matokeo hayo katika mchezo huo wa kwanza wa mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

"Simba ni timu ngumu, tangu tunakuja tulijua tunakuja kukutana na timu ngumu, kilichotokea ni kitu ambacho tulikijua, timu yangu bado ni changa, wapinzani wetu wamecheza vizuri," alisema kocha huyo.

Bao la kwanza katika mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi ambaye aliwaminya mabeki wa JS Saoura na kupiga shuti lililomshinda kipa wa klabu hiyo ya Algeria kudaka zikiwa ni sekunde chache kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza na kuwafanya Wekundu wa Msimbazi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Okwi, ambaye jana alikuwa katika kiwango cha juu, alimtengenezea pasi nzuri mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya, Meddie Kagere ambaye aliingia kuchukua nafasi ya nahodha, John Bocco aliyeshindwa kuendelea na mchezo na kufunga bao la pili dakika ya 52.

Mganda huyo alimtengenezea tena pasi nzuri ya kufunga bao la tatu Mnyarwanda huyo ikiwa ni dakika ya 67 na kuendeleza kuwapa furaha mashabiki wa Simba waliojaa uwanjani hapo kuishangilia timu yao.

Baada ya bao hilo, Simba walianza kumiliki mpira kwa kucheza pasi fupi fupi na kuwapa wakati mgumu JS Saoura ambao walionekana kuchoka, huku timu zote zikipata mapumziko ya kunywa maji katikati ya mchezo kutokana na hali ya joto iliyopo jijini.

Simba sasa wanajiandaa na safari ya kuwafuata AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao jana usiku walikuwa ugenini Misri kuwakabili wenyeji Al Ahly.

Habari Kubwa