Simu zapigwa 'stop' kambini Simba, Yanga

17Feb 2016
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Simu zapigwa 'stop' kambini Simba, Yanga
  • ***Wakati TFF ikimtangaza refa mwanamke 'kizihukumu' Simba, Yanga Jumamosi hii, klabu hizo zimewapiga 'stop' wachezaji wake kuzungumza na simu..

KAMA kawaida ya maandalizi ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kutokosa vituko, mbwembwe, fitna za kishabiki na majigambo, ndivyo ilivyotokea safari hii baada ya klabu zote mbili kuwapiga 'stop' wachezaji wao kufanya mawasilianoya simu.

YANGA

KAMA kawaida ya maandalizi ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kutokosa vituko, mbwembwe, fitna za kishabiki na majigambo, ndivyo ilivyotokea safari hii baada ya klabu zote mbili kuwapiga 'stop' wachezaji wao kufanya mawasilianoya simu.

Mabingwa Yanga wako Pemba kujiandaa na mechi hiyo, huku watani wao Simba wakiwa Morogoro.

Habari kutoka ndani ya klabu hizo zimedai kuwa wachezaji wamekatazwa kuongeza na simu kwa muda wote watakaokuwa kambini kujiandaa na mechi hiyo.

Sababu kubwa ya uamuzi huo ni kuwapa wachezaji fursa ya kuwekeza muda mwingi kufanya mazoezi badala ya kujishughulisha na simu.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba (jina linahifadhiwa), aliliambia gazeti hili jana kuwa ni vigumu kuwasiliana moja kwa moja na wachezaji.

"Tunaamini matokeo ya mchezo wa Jumamosi yatatoa mwanga wa mbio za ubingwa, hivyo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri lazima wachezaji wawekeza muda mwingi kwenye mazoezi," alisema mjumbe huyo.

Mambo yako hivyo ndani ya kambi ya Yanga na meneja wa klabu hiyo, Hafidh Saleh alisema jana kuwa Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm ameagiza utulivu na siri ndani ya kambi yao.

"Ninachoweza kusema ni kwamba, timu inaendelea vizuri na kambi, lakini siwezi kuzungumza zaidi kwa sababu kocha hataki taarifa za ndani ya kambi zitolewe nje," alisema Saleh.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wachezaji wa timu hizo kuzuiwa kuongea na simu wakati wakiwa kambini kujiandaa na mechi baina yao.

Wakati hayo yakitokea, Kocha wa Simba, Jackson Mayanja amesema kikosi chake kinakwenda kuivaa Yanga kikiwa kwenye kiwango cha juu cha kujiamini kuliko ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza, hata hivyo amesisitiza; "Kujiamini kwetu haina maana kwamba tayari kwamba wameshashinda mechi hiyo."

Yanga atakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kuifanya mechi ya marudiano kubeba taswira ya Simba kutaka kulipa kisasi.

Simba itashuka dimbani ikiwa kwenye kiwango kizuri na kufanikiwa kuongoza ligi baada ya kushinda mechi saba mfululizo.
"Ni mchezo mgumu kwa sababu unaangaliwa sana. Tunakwenda uwanjani tukiwa tunajiamini, lakini hatuwabezi wapinzani wetu Yanga, wana uwezo mkubwa," alisema Mayanja.

"Ni mechi inayoweza kutoa mwelekeo wa mbio za ubingwa, lakini hata kama tutashinda bado kuna mechi nyingi mbele."
Simba yenye pointi 45 itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United, wakati Yanga yenye pointi 43, inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika iliichapa Cercle de Joachim bao 1-0 nchini Mauritius.